Habari Mseto

Sh200m kutolewa kujenga soko la kisasa Githurai 45

September 3rd, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI kuu inapanga kujenga soko la kisasa eneo la Githurai 45 ili kupunguza msongamano uliyopo kwa sasa.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alisema tayari serikali imekubali kutumia Sh200 milioni zitakazosimamia ujenzi huo.

Zaidi ya wafanyi biashara 6,000 katika soko hilo wamekuwa na wakati mgumu huku wakifurushwa kutoka kando ya barabara ambako wamekuwa wakiendeshea biashara yao.

Serikali ya Kaunti ya Kiambu na halmashauri ya usalama wa barabara KenHa waliwafurusha wafanyi biashara hao miezi miwili zilizopita baada ya wengi wao kufurika katika barabara kuu ya Thika-Superhighway.

Akizungumza na wakazi wa Githurai mwishoni mwa wiki Bw King’ara alisema ujenzi wa soko hilo litang’oa nanga hivi karibuni na kwa hivyo hakuna haja ya kuwa na wasiwasi wowote.

“Ninajua kwa sasa wafanyi biashara wanapitia wakati magumu, lakini mtalazimika mvumilie hivyo kwa muda hadi mipango ifanywe ili mpate mahali mwafaka pa kupelekwa kwa muda,” alisema Bw King’ara.

Alisema baada ya soko hilo kukamilika itageuza maisha ya wengi kwa sababu italeta ongezeko la kazi kwa vijana wengi. Hata uhalifu utapungua kwa kiwango fulani.

“Tunaelewa wakati soko hilo lilipobomolewa watu wengi walikosa ajira hasa vijana huku wengi wakirejelea uhuni, lakini ningetaka wajue ya kwamba serikali inawajali kwa vyovyote vile,” alisema Mbunge huyo.

Hapo awali serikali ya Kaunti pia ilikuwa imetangaza kuwa ilikuwa imetenga fedha fulani kwenye bajeti yao ya mwaka 2019-20 ili kushughulikia soko hilo.

Wakazi hao wamepewa hakikisho kuwa wakati soko hilo litakapokamilika kila mmoja ni lazima awe na mahali pa kufanyia biashara yake.

Alisema serikali inataka kuona wafanyti biashara wakiendesha mambo yao kwa njia ya utaratibu bila kuingilia barabara kuu ya Thika-Superhighway.

Hata hivyo Halmashauri ya usalama wa barabara KenHA imetoa onyo kali kwa yeyote atakayepatikana akiuza vifaa vyake kando mwa barabara kuwa atashtakiwa kwa kosa hilo.