Habari Mseto

Sh48 milioni zatengwa kuwalipia karo wanafunzi 15,000 Nakuru

April 19th, 2018 1 min read

NA MERCY KOSKEY

ZAIDI  ya wanafunzi 15,000 wa shule za upili na wanaotoka kwa familia sizizojiweza watanufaika na mpango wa karo wa kaunti ya Nakuru, baada ya mradi huo kuanzishwa rasmi Alhamisi.

Hii ni baada ya serikali ya kaunti ya Nakuru kutoa zaidi ya Sh48 milioni ili kufanikisha mpango huo. Baadhi ya wanafunzi wanaolengwa ni wale wanaosomea shule za upili za mabweni.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuanzisha rasmi mradi huo, Gavana Lee Kinyanjui alitoa  tahadhari kwa walimu ambao watapatikana wakitumia pesa hizo kwa njia ambayo haipaswi kuwa watakabiliwa kisheria.

“Tutahakikisha kuwa pesa hizi zitafaidi wanafunzi ambao walichaguliwa kutoka familia ambazo hazijiwezi na kuwa haziporwi wale ambao hawakuchaguliwa” Gavana Kinyanjui akasema.

Gavana huyo aidha aliwashahuri wazazi kuwapa motisha  watoto wao watie bidii masomoni, akisema baadhi ya shule za msingi na upili hasa zile za umma matokeo yao hayadhihirishi.

Waziri wa elimu wa kaunti, Raymond Komen aliwahakikishia wazazi pamoja na walimu kuwa njia mwafaka ilitumika kuchagua wanafunzi ambao walitunzwa ili waendeleze masomo yao bila.

“Tuliweza kufuata taratibu zote ambayo ilikua inafaa kabla ya kuchagua wanafunzi hawa ambao walibahatika na mpango huu,” Komen alisema.

Virgzillah Nyanchama mwanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka shule ya upili ya Morop hakuweza kuficha furaha yake na kueleza kuwa sasa ataweza kuendelea na masomo yake bila kukatiziwa kutokana na ukosefu wa karo.

“Nitatia bidii masomoni ili niweze kujiunga na chuo kikuu na nitimize  ndoto yangu ya kuwa daktari,”akaeleza  mwanafunzi huyo.