Habari

Sh50 bilioni zaishia msituni

October 29th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI imetumia zaidi ya Sh50 bilioni kukabiliana na magaidi wa Al-Shabaab katika Msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu.

Katibu wa Wizara ya Usalama Dkt Karanja Kibicho, alifichua Alhamisi kuwa fedha hizo zimetumika katika ununuzi wa silaha ambazo zimekuwa zikitumiwa na vitengo mbalimbali vya usalama katika kukabiliana na magaidi hao.

Mnamo Septemba, 2015, serikali ilizindua operesheni kwa jina ‘Linda Boni,’ kwa lengo la kuwafurusha magaidi wa Al-Shabaab waliokuwa wakijificha ndani ya msitu huo mkubwa.

Akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Hindi jana, Dkt Kibicho alisema kutokana na oparesheni hiyo usalama katika Kaunti ya Lamu umedhibitiwa vilivyo.

Lakini licha ya oparesheni hiyo ya usalama na miradi ya maendeleo kuanzishwa, wakazi wa Lamu bado wanakumbwa na changamoto tele.

Katika Msitu wa Boni, wakazi ambao wengi wao ni wa jamii ya walio wachache ya Waboni bado wanahangaika kwa kukosa chakula cha kutosha.

Mapema wiki hii Taifa Leo ilizuru eneo hilo na kugundua kuwa wakazi wamekuwa wakiingia msituni kujitafutia matunda ya mwitu na mizizi kwa sababu ya kukosa chakula.

Kabla ya oparesheni hiyo, shule kadha zikiwemo Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe zilifungwa kutokana na mashambulizi ya Al-Shabaab.

Baada ya hali ya usalama kurejea na shule hizo kufunguliwa, masomo yamekuwa hayaendelei kikamilifu kutokana na uhaba wa walimu.

Shule hizo zinahudumia wanafunzi wa chekechea hadi darasa la nne pekee, ilhali wale wa madarasa ya juu hulazimika kuhamishwa hadi eneo la Mokowe ambalo ni mbali na Msitu wa Boni.

Changamoto nyingine inayokumba wakazi wa vijiji vingi vya Lamu ni ukosefu huduma za mawasiliano ya simu. Hii imefanya wakazi kuendelea kuishi maisha ya zamani bila kutangamana na wenzao kwenye mitandao kwani mawasiliano eneo hilo ni duni.

“Tunaziomba kampuni za mawasiliano kuweka milingoti ya mawasiliano eneo hili ili nasi tuweze kuungana na wengine katika utandawazi. Hatuwezi kujadili mambo muhimu yanayotuathiri kwani mawasiliano hapa ni duni,” akasema Bi Khadija Abatika, mkazi wa Mangai.

Vijana nao wamekuwa wakiililia serikali kuwapa ajira hasa kwenye mradi wa Lapsset kwani licha ya Lamu kuwa mwenyeji wa mradi huo, idadi kubwa ya wanaofanya vibarua ni watu kutoka kaunti zingine.

Elimu pia imekuwa tatizo kwa vijana wengi, ikizingatiwa kuwa wengi wao wameathiriwa na dawa za kulevya.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Abdul Kassim Ahmed aliiomba serikali kuwanasua vijana wa eneo hilo kupitia kuwafadhili kimasomo.

“Rais Mstaafu Mwai Kibaki alikuwa ameahidi kwamba vijana 1,000 wa Lamu watafadhiliwa kusomea kozi zitakazowawezesha kuajiriwa katika Lapsset. Miaka mingi imepita na ni vijana 400 pekee waliofadhiliwa. Ombi letu ni kwamba vijana 600 waliobakia wateuliwe kwa awamu moja na wote wawe ni kutoka Lamu ili wafadhiliwe kusomea kozi za Lapsset,” akasema Bw Kassim.

Suala la ardhi pia bado ni changamoto kwa wakazi wa Lamu.

Lakini akihutubu jana, Dkt Kibicho aliwataka wakazi kuacha propaganda kuhusu masuala ya uongozi na badala yake kuungana na serikali ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inayolengwa Lamu inafaulu.

“Ningewasihi wananchi wajitenge na matamshi ya kuwagawanya ambayo yanaonyesha kana kwamba serikali haifanyi kazi eneo hili. Ikumbukwe miaka mitano iliyopita, sehemu nyingi za Lamu, ikiwemo hapa Hindi, Mpeketoni na Boni zilikuwa hazikaliki kutokana na mashambulizi ya kila mara ya Al-Shabaab. Nashukuru kwamba kwa sasa Lamu ni salama,” akasema Dkt Kibicho.

Kauli yake iliungwa mkono na Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama, ambaye alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kujitolea kuona kwamba watu wa Lamu wanapata maendeleo na usalama.

“Tumejionea barabara zikijengwa. Bandari yetu ya Lamu pia inaendelea kujengwa. Ningewasihi watu wangu kwamba tusidanganywe,” akasema Bw Muthama.