Habari MsetoKimataifa

Shabaab 52 wauawa katika shambulizi

January 21st, 2019 1 min read

VALENTINE OBARA na AFP

WANAJESHI wa Amerika waliwaua magaidi 52 wa kundi la al-Shabaab nchini Somalia usiku wa kuamkia jana kwa kurusha mabomu kutoka angani.

Hatua hiyo ilitokea siku chache baada ya kundi hilo kufanya shambulio Nairobi, ambapo watu 21 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

“Kikosi cha wanajeshi wa Amerika kilicho Afrika kilifanya shambulio kutoka angani kukabiliana na idadi kubwa ya wanamgambo wa al-Shabaab wanaopigana na Jeshi la Kitaifa la Somalia. Kwa sasa tunaweza kuthibitisha shambulio hili liliua magaidi 52,” ikasema taarifa kutoka kwa kikosi hicho.

Maafisa wa kijeshi na wazee wa jamii za Somalia, walisema magaidi wa al-Shabaab wenye silaha kali walikuwa wameanzisha shambulio katika kambi ya jeshi la nchi hiyo ndipo makabiliano ya kufyatuliana risasi yakaanza na kudumu kwa saa nyingi.

“Magaidi walikuwa wamevamia kambi ya kijeshi ya Bulogagdud wakiwa na silaha kali na vilipuzi. Jeshi la Somalia na wale wa Jubaland walikabiliana na maadui kabla ya kurejea katika kambi yao,” Mohamed Abdikarin, ambaye ni afisa wa jeshi la Somalia aliambia AFP kwa simu.

Aliongeza: “Wanajeshi sita waliuawa kwenye shambulio hilo na wengine wawili wakafa wakati gari lililojazwa mabomu lilipolipuliwa.”

Duru katika vijiji vya karibu zilisema magaidi hao walipora mali katika kambi ya kijeshi, ikiwemo gari la wanajeshi.

“Waliteka usimamizi wa kambi hiyo na wakaiba kila kitu. Wamechoma hifadhi za silaha na wakachukua gari la kijeshi lakini ndege ya kivita ikawashambulia kutoka angani,” mzee wa kijamii, Hassan Rashid aliambia AFP.

Shahidi mwingine, Sulayman Isse, ambaye alikuwa katika kijiji cha karibu wakati wa makabiliano hayo, alisema baadaye wanajeshi wa Somalia walijikusanya upya wakarudi kambini baada ya wenzao kujiunga nao kutoka Kismayo.

“Wanajeshi wa Somalia walidhibiti upya kambi yao walipopata usaidizi kutoka kwa ndege za kijeshi zinazomilikiwa na jeshi maalumu la Amerika ambazo zilikuwa zikipepea eneo hilo hata baada ya shambulio,” akasema.