Michezo

Shabana FC katika hatari ya kusambaratika

July 13th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANASOKA wengi wa Shabana FC wamewasilisha maombi ya kuagana rasmi na kikosi hicho kinachotishiwa na hatari ya kusambaratika kutokana na hali ngumu ya kifedha.

Kwa mujibu wa Jared Sani ambaye ni meneja wa timu, takriban robo tatu ya wachezaji wa kikosi cha kwanza wametaka kuachiliwa ili watafute hifadhi kwingineko.

Watatu kati ya wachezaji hao 15 wanaolenga kuondoka, wanahusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya Gusii FC, kikosi kinachoshiriki kipute cha Daraja la Kwanza la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) chini ya mkufunzi Paul Mayieko ambaye ni mwenyeketiki wa zamani wa Shabana FC.

“Baadhi ya wachezaji wamewasilisha barua za kutaka kuachiliwa. Matamanio yao ni kujiunga na vikosi vingine kwa minajili ya kampeni za muhula ujao. Hii ni hali tata zaidi kwa usimamizi wa Shabana FC,” akatanguliza Sani.

“Kikosi kilipitia changamoto tele msimu uliopita. Hata hivyo, ningependa kushukuru usimamizi na mashabiki kwa kuhakikisha kwamba tunashiriki mechi zote licha ya panda-shuka ya kifedha zilizotishia kututikisa,” akaongeza.

Sani amesema kwamba wengi wa wanasoka wake wamekuwa wakijifanyia mazoezi nyumbani huku wengine sita wakiondoka kambini Jumanne iliyopita baada ya baadhi ya masharti yanayodhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kulegezwa.

Wanasoka wa zamani wa Shabana FC chini ya uongozi wa Peter Kamau, wameahidi kusaidia kikosi hicho kurejesha makali ya zamani. Mbali na kuahidi kutafuta mdhamini, wametaka kikosi kiwe na usimamizi thabiti na mpangilio bora utakaowasaidia kupanda ngazi hadi kushiriki Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Nyandoro Kambi ambaye ni Naibu Mwenyekiti, amefichua mpango wa kuandaliwa kwa mkutano mwezi ujao ili kuwapa washikadau jukwaa mwafaka la kutoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kukisuka upya kikosi cha Shabana FC.