Michezo

Shabana yapigwa na Ulinzi ugani Raila Odinga

January 20th, 2024 1 min read

Na WYCLIFFE NYABERI

MASAIBU ya klabu ya Shabana FC katika Ligi Kuu ya Kandanda nchini (FKF-PL) yanazidi kuongezeka baada ya timu hiyo kukung’utwa 1-0 na wanajeshi Ulinzi Stars katika mchuano uliogaragazwa Jumamosi katika uwanja wa Raila Odinga mjini Homa Bay.

Bao hilo la pekee lilitingwa kimiani katika dakika ya kwanza kupitia mchezaji Masuta Masita baada ya kupokezwa pasi murwa kutoka kwa kiungo Leshan Mootian.

Baada ya kuchukua uongozi huo, Ulinzi walicheza kwa tahadhari sana katika mchezo wote na waliibuka na alama zote tatu baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa.

Matokeo hayo yanaiacha Shabana katika nafasi ya 17 na alama 17, tatu mbele ya Nzoia Sugar inayoburuta mkia jedwalini.

Baada ya kujimwaya uwanjani mara 19, vijana hao wa kocha Sammy Omollo ‘Pamzo’ wameshinda mechi nne, wakatoka sare tano na kupigwa mara 10.

Pamzo aliteuliwa kocha wa timu hiyo maarufu kama ‘Tore Bobe’ mapema mwaka huu 2024 na kupewa jukumu la kuiondoa kutoka kwa eneo hatari la kushushwa ngazi.

Katika mchezo wake wa kwanza akiwa usukani wikendi iliyopita, kocha huyo mzoefu aliiongoza timu yake kuikomoa Nzoia Sugar mabao 5-2.

Mechi hiyo ilichezewa Bungoma katika uwanja wa Sudi.

Kwenye matokeo mengine ya mechi zilizogaragazwa Jumamosi, vinara Gor Mahia walizidi kung’aa baada ya kuwashinda Tusker FC kwa kuwafunga 1-0.

Bandari na Kariobangi Sharks ziliumiza nyasi kwa kufungana 2-2 ilhali KCB na Muhoroni Youth ziliambulia sare tasa.