Michezo

Shabiki wa Man City ashambuliwa na mashabiki wa Schalke 04

February 21st, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

UONGOZI wa Manchester City umetangaza kwamba shabiki wao mmoja yupo hali mahututi hospitalini baada ya kushambuliwa kufuatia ushindi wa 3-2 dhidi ya Schalke 04 nchini Ujerumani Jumatano usiku.

Tukio hilo lilijiri baada ya ngarambe kali ya mkondo wa kwanza kati timu hizo zinazowania kufuzu hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Barani Uropa(UEFA).

“Manchester City wanafahamu habari za kuvamiwa na kupigwa kwa shabiki wao baada ya mechi iliyoandaliwa uwanja wa Veltins, Ujerumani Jumatano usiku. Klabu inashirikiana na maafisa wa polisi jijini Manchester na wenzao kutoka Ujerumani kudadavua tukio hilo,”

“Maafisa wa timu wamesalia Ujerumani ili kuipa sapoti familia ya mwathiriwa ambaye yupo katika hali mahututi. Mtu yeyote aliye na habari muhimu kuhusu uvamizi huo anaombwa awaarifu polisi kwa kupiga simu kwenye nambari 101,” ikasema taarifa ya mabingwa hao watetezi wa LIgi Kuu ya Uingereza(EPL).

Uwanjani, Man City walishuhudia miujiza walipotoka nyuma na kushinda Schalke O4 3-2, ushindi ambao unawawezesha kutia guu moja ndani ya robo fainali wakisubiri kuandaa mkondo wa pili ugani Etihad nchini Uingereza mwezi ujao wa Machi.

Mshambulizi Nabil Bentley aliwafungia wenyeji penalti mbili huku Sergio Aguero, Leroney Sane na Raheem Sterling wakifunga mabao matatu yaliyowavunia ushindi ugenini.

Mlinzi wa Man City Nicholas Otamendi hata hivyo alionyeshwa kadi mbili za manjano na kutimuliwa uwanjani katika kipindi cha pili na hatua iliyoilazimisha timu yake kumaliza mechi wachezaji 10 uwanjani.

Hata hivyo tukio hilo si geni katika fani ya soka. Mwaka wa 2018, shabiki wa Liverpool nusura apoteze maisha yake alipohusika kwenye ajali ya barabarani akiwa na mashabiki wa AS Roma FC kabla ya mechi ya nusu fainali kati ya timu hizo kwenye kipute hicho hicho cha UEFA.

Mapema mwaka wa 2019, mashabiki wawili wa Chelsea walivamiwa nchini Ugiriki kabla ya mechi ya ligi ya Uropa iliyowakutanisha na PAOK Salonika ya taifa hilo.