Michezo

Shabiki wa Zoo aliyewatisha wapinzani kwa bastola taabani

September 18th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KAMPUNI inayoendesha ligi ya kuu nchini KPL imeanzisha uchunguzi kuhusu kisa kilichoshuhudiwa Jumapili Septemba 16 wakati shabiki wa Zoo Kericho alitoa bastola na kutishia kuwapiga risasi wachezaji wa Bandari katika sare ya 1-1 katika uwanja wa Kericho Green Stadium.

Tukio hilo limechoma sura ya KPL na waandalizi wa mechi hiyo na kupelekea  huduma za polisi kushirikishwa katika uchunguzi huo unaolenga kutegua kitendawili kilichopelekea kutokea kwa kisa hicho.

“KPL inaomba kuwajuza wadau katika fani ya soka na umma kwa jumla kwamba wameanzisha uchunguzi  kuhusu tukio la kusikitisha la jaribio la ufyatulianaji wa risasi ambalo lilihusisha shabiki anayedaiwa kuwa afisa wa polisi na wachezaji wa Bandari FC katika uga wa Kericho Green Stadium Jumapili Septemba 16,2018 baada ya mechi ya ligi ya Sportpesa, 2018 raundi ya 30 kati ya Zoo Kericho FC na Bandari,” ikasema taarifa katika mtandao wa KPL..

Aidha kampuni hiyo iliahidi kuchunguza kwa kina kisa hicho na kuhakikisha watakaopatikana na hatia wanaadhibiwa kwa kuipaka tope mchezo unaohusudiwa wa kandanda.

Vile vile iliahidi kwamba itaandikia Inspekta Mkuu wa polisi kuingilia swala hilo kwa lengo la kuhakikisha maafisa wake wa usalama walioidhinishwa kumiliki bunduki wanazitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mechi hiyo iliyojaa hisia na vimbwanga ndani na nje ya uwanja  ilivutia mamia ya mashabiki walioshangilia sana timu ya nyumbani.