Shahbal apuuza ‘jeshi’ la Nassir

Shahbal apuuza ‘jeshi’ la Nassir

Na VALENTINE OBARA

MFANYABIASHARA Suleiman Shahbal, anayepanga kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao, amepuuzilia mbali hatua ya wabunge wa eneo hilo kuungana kupinga azimio lake.

Bw Shahbal amejiandikisha kupigania tikiti ya Chama cha ODM kuwania kiti cha Gavana Hassan Joho ambaye atakamilisha kipindi chake cha pili cha ugavana mwaka ujao.Tikiti ya chama hicho inawaniwa pia na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi.

Wabunge wanachama wa ODM Mishi Mboko (Likoni), Bady Twalib (Jomvu), Seneta Mohamed Faki, na Mbunge Mwakilishi wa Kike, Bi Asha Mohamed waliungana na Bw Nassir kupiga kampeni kwa miezi kadhaa sasa, hali iliyomwacha Bw Shahbal pweke.

Wabunge hao pia hudhibiti ziara za Kiongozi wa ODM Raila Odinga eneo hilo.Kulingana na Bw Faki, waliamua kumuunga mkono Bw Nassir kwa vile ashaonyesha uaminifu wake kwa chama na utendakazi bora.

“Kama nilipambana na Ali Hassan Joho tukaendeshana ‘mundu khumundu’ acha hao wengine waje sasa,” Bw Shahbal alisema katika mkutano wa kisiasa wikendi, mtaani Old Town.Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Bw Shahbal kuwania ugavana Mombasa, baada ya kujaribu mwaka wa 2013 kupitia Chama cha Wiper na 2017 kupitia Jubilee ambapo aliibuka nafasi ya pili.

Katika mahojiano ya awali, Bw Shahbal alisema kizingiti chake kushinda awali ilikuwa ni Bw Joho kwa hivyo sasa ana matumaini makubwa kuwa gavana wa pili wa mji huo wa kitalii.Huku akionekana kuwalenga wapinzani wake, aliwataka wananchi kujihadhari na wanasiasa ambao hawana mikakati mwafaka ya kuendeleza mbele mji huo.

Alisema uamuzi ambao wananchi watafanya 2022 kuhusu uongozi wa kaunti hiyo, utaamua kama Mombasa itasonga mbele kimaendeleo ama itapiga hatua nyuma.“Kila mwaka wakati wa uchaguzi watu huja kusema wataleta maendeleo lakini hawaelezi jinsi wanapanga kubadilisha huu mji.

Hawaelezi mikakati ya kusaidia nchi ipate kuendelea,” akasema.Tofauti na wanasiasa wengine ambao hufanya mikutano ya hadhara kuuza sera zao, Bw Shahbal amekumbatia mtindo wa kufanya mikutano mabarazani na makundi mbalimbali ya kijamii.

Kulingana naye, mtindo huo humwezesha kupokea maoni na maswali ya wananchi ili kuyajumuisha katika mipango yake ya uongozi.“Nimezunguka mji mzima kueleza mawazo yangu na kusikiliza mawazo na maswali ya mwananchi kwa sababu kila mtu ana maoni yake yanayoweza kusaidia kimaendeleo,” akasema.

Bw Shahbal alirejelea ahadi yake ya kupendekeza bunge la kaunti liidhinishe kuwa Sh50 milioni za maendeleo ziwe zikipeanwa kwa kila wadi endapo atashinda uchaguzi ujao.Kwa sasa, Serikali ya Kaunti hukubaliwa kupeana kiwango chochote kisichopungua Sh26 milioni kwa kila wadi katika kila mwaka wa kifedha.

You can share this post!

Jamii mbioni kulinda afya ya mama na mtoto

MARY WANGARI: Mauaji ya Tirop ni uhalisia mchungu wa janga...

T L