Habari MsetoSiasa

Shahbal atetea mikutano na Raila, alenga ugavana 2022

June 18th, 2020 1 min read

Na MOHAMED AHMED

MFANYABIASHARA wa Mombasa, Bw Suleiman Shahbal ametetea mikutano yake ya mara kwa mara na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga.

Huku akithibitisha azimio lake kuwania ugavana Mombasa katika uchaguzi ujao, Bw Shahbal ambaye ni mwanachama wa Jubilee alidai kwamba mikutano hiyo huwa ni ya kimaendeleo wala si kujiandaa kisasa.

“Kwa sababu ya umoja wa viongozi wetu, mimi huenda kumuona kwa sababu ya mipango ya maendeleo. Hii ni fursa ya kukutana na kiongozi kama yeye,” akasema.

Mkutano wao wa hivi karibuni ulikuwa wiki iliyopita ambapo alimtembelea Bw Odinga afisini mwake.

Kulingana na wadokezi wetu, Bw Shahbal anatazamiwa kuingia kwenye muungano wowote ambao utasimamiwa na Bw Odinga ifikapo mwaka wa 2022.

Endapo atapitishwa na Bw Odinga, inaaminika Bw Shahbal atapata mwanya mkubwa kushinda kiti hicho. Anatazamiwa kupambana na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir na mwenzake wa Kisauni Ali Mbogo.

Bw Nassir amekuwa mwandani wa kisiasa wa Gavana Hassan Joho kwa muda mrefu lakini kwa miezi kadhaa sasa, Bw Shahbal pia ameonekana akinyemelea upande wa Bw Joho.

“Mwaka wa 2022 bado uko mbali. Kwa sasa kiti hicho kina mwenyewe ambaye ni Gavana Joho, kwa hivyo ni lazima tushirikiane naye kwa ajili ya kaunti yetu,” akasema Bw Shahbal.

Alikuwa akizungumza katika Shule ya Spaki ambao alizindua mradi wa masomo.

“Tusiweke kaunti hii katika hali ya kampeni wakati kampeni bado hazijafika. Kwa sasa ni ushirikiano wa maendeleo ndio muhimu. Siasa bado miaka miwili ijayo,” akasema Bw Shahbal.