Shahbal atetea mradi wa nyumba Buxton

Shahbal atetea mradi wa nyumba Buxton

Na VALENTINE OBARA

MFANYABIASHARA Suleiman Shahbal, anayepanga kuwania ugavana Mombasa, ameomba maseneta wasitumiwe kisiasa kukwamisha mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa katika mtaa wa Buxton.

Mradi huo unaoendelezwa na kampuni yake kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa na ile ya Kaunti ya Mombasa umekuwa ukipingwa na baadhi ya wakazi na viongozi wanaodai unatekelezwa kwa usiri ilhali ardhi inayotumiwa ni ya umma.

Malalamishi mengine yaliyoibuka ni kuwa, huenda wakazi waliohamishwa katika nyumba zilizobomolewa hawatapewa nafasi ya kumiliki nyumba mpya zitakapokamilishwa kujengwa. Ujenzi huo unatarajiwa kugharimu Sh6 bilioni.

Miezi michache iliyopita, Kamati ya Seneti inayosimamia masuala ya barabara, uchukuzi na miundomsingi iliagiza ujenzi usitishwe hadi wanaoendeleza mradi huo wajibu malalamishi yaliyoibuka.

Hata hivyo, agizo hilo lilipuuzwa. Katika mahojiano na wanahabari Jumatatu, Bw Shahbal alilalamika kuwa pingamizi zinazoelekezwa kwa mradi huo ni kutokana na wanasiasa wanaopinga azimio lake la kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho.

Alimlaumu Seneta wa Mombasa, Bw Mohamed Faki, kwa kuwasilisha barua katika seneti ili mradi huo uchunguzwe ilhali, kulingana naye, seneta huyo alikuwa ameshiriki katika vikao vya kupokea maoni ya umma awali.

“Seneti ilikuwa na maswali, wakajibiwa kwa hivyo mradi waendelea. Kamati ya seneti inachochewa na wanasiasa wa Mombasa. Huu mradi ulianza mnamo 2015 ukapitishwa na bunge la kaunti ilhali malalamishi yanaibuka wakati huu,” akasema.

Bw Faki ni mmoja wa wanasiasa wa ODM Mombasa ambao wanaunga mkono azimio la Bw Nassir kwa ugavana.

You can share this post!

Raila alilia vijana Nyanza wajisajili kwa kura za 2022

Ndume 3 ulingoni kwa ndondi za Serbia

F M