Shahbal awapuuza wakosoaji

Shahbal awapuuza wakosoaji

NA ANTHONY KITIMO

MFANYABIASHARA Suleiman Shahbal, amepuuzilia mbali mahasimu wake wanaotilia shaka kama ataweza kuwa mwadilifu iwapo atachaguliwa kuwa gavana wa pili wa Mombasa katika uchaguzi ujao.

Bw Shahbal, ambaye anamezea mate tikiti ya Chama cha ODM kushindania ugavana, amekuwa akikashifiwa na baadhi ya wapinzani wake kwa vile ndiye alipewa kandarasi na kaunti kujenga nyumba mpya za bei nafuu katika mtaa wa Buxton.

Akizungumza Jumatano katika hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa na shirika la Rotary mjini humo, alisema mradi huo utakamilika kwa wakati unaofaa, na ana mipango ya kuanzisha miradi mingine kama hiyo iwapo atashinda ugavana ila hataomba kandarasi.

“Tutaonyesha wakazi wa Mombasa kwamba kukiwa na mipango mizuri, watu wanaweza kuishi katika makazi nadhifu kwa bei nafuu. Nitakapochaguliwa, tutaendeleza miradi mingine ya nyumba kama hizi na mimi wakati huo nitakuwa msimamizi tu, sitaomba hata kandarasi moja katika kaunti,” akasema.

Wiki iliyopita, seneta wa zamani wa Mombasa, Bw Hassan Omar, alidai kuwa kandarasi hiyo ya Buxton inaweza kumwangusha vibaya Bw Shahbal uchaguzini.

Kulingana naye, hii ni kutokana na vile mradi huo ulikumbwa na mizozo mingi kabla uzinduliwe na vile vile, baadhi ya wakazi wanajiuliza jinsi mfanyabiashara huyo ataweza kutenganisha biashara zake na usimamizi wa kaunti iwapo wataamua wamchague kuwa gavana.

Katika mahojiano na kituo cha redio mjini humo, Bw Omar ambaye ananuia kuwania ugavana kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA), alisema wanaamini mshindani wao atakuwa ni mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, ambaye pia anasaka tikiti ya ODM.

Tikiti ya ODM yatafutwa pia na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi.

Hata hivyo, Bw Shahbal alisema kwamba ameweka mikakati ya kutosha kushindania tikiti ya ODM katika kura ya mchujo.

Kulingana naye, kampeni zake mashinani na mifano ya miradi ambayo anatekeleza ni dhihirisho kuwa yuko tayari kuongoza Kaunti ya Mombasa.

“Wakati Rais Uhuru Kenyatta alikuwa anafanya handisheki na kinara wa Chama cha ODM Raila Odinga, mimi na gavana wa Mombasa tulikuwa tunafanya yetu mashinani na mfano mzuri ni mradi wa nyumba za Buxton ambazo ni dhihirisho kuwa kila kitu kinawezekana,” akasema.

Katika hafla ya Jumatano iliyohudhuriwa na wafanyabiashara mbalimbali wa Mombasa, mwaniaji huyo alisema yeye yuko tayari kufanya kazi na watu kutoka sekta tofauti ili kuboresha Mombasa na kupunguza kutegemea ufadhili wa miradi kutoka kwa serikali ya kitaifa.

“Mimi nimezuru nchi mbalimbali na nina wafadhili ambao wako tayari kuwekeza mjini Mombasa ndiyo maana niko hapa kuomba tushirikiane ikizingatiwa kuwa wengi wameona kazi yangu katika sekta mbalimbali ambazo nimefanya kazi nao,” akasema Bw Shahbal.

Mfanyabiashara huyo pia ameendeleza kampeni kuhakikisha wakazi wamejiandikisha kuwa wapigakura na kumchagua Bw Odinga kuwa rais katika uchaguzi mkuu ujao.

Amekuwa akitumia mikakati ya kukutana na wanachama wa ODM mashinani ili kupata uungwaji mkono dhidi ya mpinzani wake wa karibu Bw Nassir ambaye naye pia anajipigia debe kutafuta tikiti hiyo.

Bw Nassir amepata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wa ODM katika Kaunti ya Mombasa, kando na kuwa mwandani wa karibu wa Bw Joho ambaye huashiria kumuunga mkono.

You can share this post!

Wabunge kukutana tena Jumanne kufufua hoja iliyozimwa na...

Hasara upepo ukizidisha dhoruba Bahari Hindi

T L