Shahbal hatimaye aingia ODM

Shahbal hatimaye aingia ODM

Na VALENTINE OBARA

MWANASIASA Suleiman Shahbal hatimaye amejisajili rasmi kujiunga na Chama cha ODM na hivyo basi kuepuka hatari ya kuzuiwa kuwania tikiti ya chama hicho kwa uchaguzi wa ugavana Mombasa mwaka ujao.

Usajili wa mfanyabiashara huyo kujiunga na chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, ulikuwa umecheleweshwa na kanuni alizofaa kufuata kabla kuhama Chama cha Jubilee.

Mapema mwaka huu, Kamati Kuu ya Kitaifa ya ODM (NEC) ilipitisha uamuzi kuwa mtu yeyote anayepanga kutumia chama hicho kuwania kiti cha kisiasa mwaka ujao lazima awe amejisajili kuwa mwanachama wa daima mwaka mmoja kabla uchaguzi ujao ufanywe.

“Alijisajili mara moja baada ya afisi ya msajili wa vyama kuthibitisha kuwa ombi lake la kutaka kuondolewa katika sajili ya Jubilee liliidhinishwa,” akasema afisa anayesimamia mawasiliano yake kwa umma, Bw Mohamed Ahmed.

Kikatiba, Uchaguzi Mkuu ujao unapaswa kufanyika Agosti 9, kwa hivyo wanaotaka tikiti za chama hicho wamebaki na muda mfupi isipokuwa kama ODM itabadili msimamo wake kuhusu uamuzi wa awali.

“Tungependa kuwajulisha wawaniaji wanaotarajia kutumia tikiti ya chama hiki kwamba wana muda hadi Agosti mwaka huu kujisajili kuwa wanachama daima wa ODM,” chama hicho kilisema kwenye taarifa baada ya NEC kufanya uamuzi huo Februari.

Hatua hiyo ilichukuliwa kama mojawapo ya mbinu za kuepusha malalamishi kwamba vyeti vya uteuzi hupeanwa kwa wanasiasa wasio waaminifu kwa chama.

Wanasiasa hao hudaiwa kujiunga na chama dakika za mwisho na kutumia ushawishi wao kushinda katika kura ya mchujo kisha baadaye hukisaliti baada ya kushinda vyeo uchaguzini.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa walidai kuwa huenda uamuzi huo wa ODM ukawafungia nje pia watumishi wa umma ambao wangependa kujitosa katika siasa mwaka ujao kwani kisheria, hawafai kuegemea upande wowote wa kisiasa.

Katika cheti cha kuthibitisha malipo yake kujiunga na ODM ambayo Taifa Leo iliona, Bw Shahbal alilipa Sh20,000 kuwa mwanachama wa daima wa chama hicho.

Anatarajia kuwania ugavana Mombasa mwaka ujao iwapo atashinda tikiti ya ODM dhidi ya Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir.

Wawili hao ni miongoni mwa wanasiasa wengine wanaomezea mate kiti cha ugavana kitakachobaki wazi wakati Gavana Hassan Joho atakapokamilisha kipindi chake cha pili 2022.

Wiki iliyopita, Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka alitoa wito kwa wanachama wa zamani akiwemo Bw Shahbal kurudi kwa chama hicho kinapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao.

Wito wa Bw Musyoka ulitokea wakati ambapo ilikuwa imefichuka mfanyabiashara huyo alikuwa hajawasilisha rasmi ombi la kujiunga na ODM.

Bw Shahbal alikuwa ameambia Taifa Leo kwamba alicheleweshwa na baadhi ya masharti ya kisheria ambayo mtu huhitajika kukamilisha kabla jina lake kuondolewa katika sajili ya chama ambacho angependa kuhama.

Alikuwa ametumia Chama cha Wiper kuwania ugavana Mombasa katika uchaguzi wa 2013, akahamia Jubilee wakati wa uchaguzi wa 2017.

Bw Joho ndiye aliibuka mshindi katika chaguzi hizo mbili kupitia kwa ODM.

You can share this post!

Messi kuondoka Barcelona

Aliyemuua Rais Museveni mitandaoni anaswa Uturuki