Makala

Shahidi kigugumizi alivyomwokoa ajuza Rael Mayaka kuepuka jela

February 5th, 2024 2 min read

RUTH MBULA NA LABAAN SHABAAN 

SHAHIDI kigugumizi katika kesi ya mtoto Junior Sagini anadaiwa kusaidia mshukiwa, Rael Mayaka, kuachiliwa huru.

Jaji Waweru Kiage alisema upande wa mashtaka, baada ya kujua mapema changamoto iliyomkabili shahidi aliyetambuliwa kama PW11, ulikuwa na jukumu kutafuta maoni ya mtaalamu kuhusu kiasi cha zingatio ambacho mahakama ingefaa kuweka kwa ushahidi wake.

“Pia nilitarajia upande wa mashtaka uorodheshe huduma za mkalimani wa lugha ya ishara, ambayo haukufanya. Mahakama ya iliachwa kujiamulia hii. Hii si kazi rahisi. Nilikutana na maandishi ya ushahidi wa watu wenye udumavu wa akili,” alisema Jaji Kiarie.

Maandishi hayo yalisema kuwa ushahidi uliotolewa kortini na mashahidi wenye udumavu wa akili unafaa kutathminiwa.

Kabla ya kutoa ushahidi, upande wa mashtaka uliomba utambuzi wa shahidi uwekwe siri.

“Shahidi ni kigugumizi. Kiwango chake cha urazini kiko chini ya wastani. Alitumia sana lugha ya ishara. Hata hivyo, ana uwezo wa kuzungumza licha ya changamoto. Anaweza kutoa ushahidi,” upande wa mashtaka uliambia korti.

Ushahidi wake ulikuwa mkatarufaa, Mayaka, hakuhusika katika kuwasaidia wenzake kumweka kwenye gunia mlalamishi (Junior Sagini) baada ya kung’olewa macho.

Lakini Jaji Kiarie alisema kwamba ingawa PW11 alikuwa shahidi mwenye uwezo, “Wakati wa kuchambua ushahidi wa shahidi huyu, nitafuta ushahidi wa kuthibitisha kwani upande wa mashtaka ulishindwa kumpa shahidi utathmini wa kitaalamu ambao mahakama ingeweza kutumia kama mwongozo.”

Zaidi ya hayo, hakimu alibainisha kuwa ushahidi wa PW11 pia ulitoa taswira ya kuwepo kila mahali.

“Hakuna ushahidi wa kuunga mkono shtaka dhidi ya aliyekata rufaa uliotolewa, na hakuna hata mmoja uliotolewa kuthibitisha alisaidia kutekeleza uhalifu. Bila ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha ushahidi huo, haikuwa salama kutegemea ushahidi kumfunga mshukiwa,” alibainisha hakimu.

Kisha hakimu akaongeza, “Kwa hivyo, hukumu ya mrufani imefutwa. Anaachiliwa huru isipokuwa vinginevyo ashikwe kisheria.”

Mayaka, 80, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela na mahakama ya Kisii kwa madai ya kumng’oa macho mjukuu wake, Sagini.

Jaji Kiarie, akimwachilia Mayaka, alisema upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo bila mashaka yoyote.

Mayaka alitupwa gerezani pamoja na bintiye Pacificah Nyakerario na mjukuu mwingine Alex Maina Ochogo mnamo Juni 2023.

Ochogo (binamu wa Sagini), Nyakerario (shangazi ya Sagini) na Mayaka (nyanyake Sagini) walihukumiwa kifungo cha miaka 40, 10 na 5 mtawalia, kwa kuripotiwa kumng’oa macho mvulana huyo wa miaka mitatu.

Ochogo na Nyakerario hawakukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.