Shahidi wa kesi dhidi ya Gicheru ICC ‘atoweka’

Shahidi wa kesi dhidi ya Gicheru ICC ‘atoweka’

Na VALENTINE OBARA

MMOJA wa mashahidi aliyetarajiwa kutoa ushahidi dhidi ya wakili Paul Gicheru katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ametoweka, kulingana na upande wa mashtaka.

Hayo yalifichuka wakati Naibu Kiongozi wa Mashtaka, Bw James Stewart, alipowasilisha ombi kutaka mahakama imruhusu kutumia taarifa za mashahidi 13 zilizokusanywa awali.Taarifa hizo zilikuwa zimekusanywa wakati wa kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 iliyomkabili Naibu Rais William Ruto.

Baadhi ya taarifa hizo ni za mashahidi waliojiondoa katika kesi ya Dkt Ruto na mwanahabari Joshua Sang, huku nyingine zikiwa za wapelelezi ambao walihusika katika uchunguzi wa ghasia zilizotokea.

Imebainika kuwa, mmoja wa mashahidi aliyebandikwa jina P-0397 kwa ulinzi wake alijiondoa katika kesi ya Dkt Ruto mwaka wa 2013.Stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani zilionyesha kuwa, alianza tena kuwasiliana na upande wa mashtaka katika mwaka wa 2014 akihofia usalama wake.

Ni katika mwaka huo ambapo alikubali kuhojiwa kuhusu mbinu ambazo inadaiwa Bw Gicheru na washirika wengine wa Dkt Ruto walitumia kuwashawishi mashahidi kukoma kushirikiana na ICC.

Alitarajiwa kuwa mmoja wa mashahidi ambao wangetoa ushuhuda wao mahakamani dhidi ya Bw Gicheru.Imedaiwa Bw Gicheru alikuwa katika kikundi cha watu waliohonga mashahidi kwa niaba ya Dkt Ruto ili wasishirikiane na upande wa mashtaka.

Upande wa mashtaka umesema haukutarajia shahidi huyo kutoweka kwa vile alikuwa ameanza kushirikiana na ICC na hata akahamishwa kwa usalama wake.“Juhudi za kutosha zilifanywa kumtafuta ili afike mahakamani, lakini ushahidi uliokusanywa kwake awali pia unaweza kuaminika,” akasema Bw Stewart.

Bw Gicheru alijisalimisha katika ICC mwaka uliopita, akakanusha madai kuwa alihusika katika njama za kuhonga mashahidi ambao walitegemewa na upande wa mashtaka katika kesi zilizohusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kesi hizo zilisitishwa wakati upande wa mashtaka ambao wakati huo uliongozwa na Bi Fatou Bensouda, uliposema hakuna ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi kwa vile mashahidi waliotegemewa walijiondoa.

You can share this post!

Ufugaji wa nguruwe unavyompa mkulima kipato Mwatate

Papa Francis ateua Askofu Anyolo kumrithi Njue

T L