Makala

SHAIRI:  LEO  NAWATUNGA!

March 2nd, 2018 1 min read

Na Mshairi Machinga 

SITAWAONEA haya, majagina kuwatunga, 

Sitatamka mabaya, Japo domo sitafunga, 

Mwaweka wino manyoya, Kuku ageuke Kanga,

Leo nawatunga!

 

Nianze na yule jini, ajiitae Kinyonga,

Alisema kwa yakini, anatafuta mganga,

Kule Arusha sinoni, waganguzi wako Vanga,

Leo nawatunga !

 

Wapi mmejionea, Teja kapata bahati,

Sawa na kutarajia, Tembo kufa kwa manati,

Yani nimewapania, mtachomekea koti,

Leo nawatunga !

 

Na yule Rasi saidi, anayetafuna nyama,

Namwambia asizidi, kilingeni kuzizima,

Asilete ukaidi, aje hapa hima hima,

Leo nawatunga!

 

Yupo kijana mmoya, rakabu kalamu ndogo,

Tungo zake sio mbaya,mjini zaleta zogo,

Eti katunga riwaya, ya mtu muuza figo,

Leo nawatunga!

 

Tangu lini wanagenzi, sumu ile kuwa tamu,

Vipi yatungwe mapenzi, yaachwe mambo adhimu,

Iweje kesi ya panzi, kunguru awe hakimu,

Leo nawatunga!

 

Kaka Hassani Moroa, mimi tenzi nazipanga,

Sitoacha kuongea ,hata wakishika panga,

Ona wananizomea, wanasema naboronga,

Leo nawatunga!

 

Shughuli wa mwashughuli, watufunza maadili,

Watuonjesha asali, haujazi bilauli,

Kitabu bila usuli, vipi kipewe kibali?

Leo nawatunga!

 

Malenga wa migombani, mkekani sikuoni,

Mashairi ukighani, watoa nyoka pangoni,

Rudi shujaa vitani, usibaki  uvunguni,

Leo nawatunga!

 

Ndugu Ali Sufiani, kijana toka Pangani,

Nilishafika Funguni, Madanga, Boza na Bweni,

Uje kutoka mwituni, acha kukimbiza nyani,

Leo nawatunga!

 

Chotara wa kizigua, wapi umejifungia,

Ngomani nishaingia, huku nikikutambia,

Vipi vumbi la mkaa ?, lifubaze sufuria,

Leo nawatunga!

 

Utafutae wazuri, wenye shepu utakayo,

Unaicheza kamari, yenye kuumiza moyo,

Shemeji kwepa ajari, usiikimbize toyo,

Leo nakutunga!

 

Mwisho ninamalizia, kuwachachafya wahenga,

Ujumbe nawaletea, namtuma njiwa manga,

Majibu nasubiria, nikitazama luninga,

Leo nawatunga!

 

Mshairi Machinga 
0716541703/0677620321,
Dar es salaam, Bongo.