Habari MsetoMashairi

SHAIRI: Tumpe jina gani?

August 26th, 2019 1 min read

Tunasaka jina lake, kiumbe al’e mgeni,

Mie pia na mamake, mengi twayatathimini,

Yapo majina ya kike, ya leo na ya zamani,

Nishauri kwenye jina, tumuite tumudeke.

 

Sanura au Sunira, majina tuloyapanga,

Samira ama Subira, lipi jema manyakanga?

Zuena, Zena na Zera, au Zuhura wa Tanga?

Nishauri kwenye jina, Zubeida na Zahira.

 

Tamara hata Tamira, Talia na Tamrina,

Vipi Lena na Laura, Leyla hata Liana?

Nambie kuhusu Lara, Tiana na Tatiana,

Nishauri kwenye jina, Lamania au Lina?

 

Tanasha au Natasha, Maisura na Melissa,

Vipi Aisha na Asha, Faiza ama Hamissa?

Maria, Mima na Masha, Naima ama Farissa,

Nishauri kwenye jina, Talisa au Vanessa?

 

Ninasihi kwa Ashura, Asinati na Latifa,

Nomba pia Shakira, Aliya hata Hanifa,

Kayla ama Debora, Noelina na Shanifa,

Nishauri kwenye jina, Nadiya au Shalifa?

 

Sijasahau Munira, Maya, Muna na Rukiya,

Sonia, Siena, Sara, Maimuna na Radhiya,

Vipi Rita na Tahira, Amrina na Raniya?

Nishauri kwenye jina, Amara, Mira na Miya.

 

Vipi kuhusu Jamila, Julia na Juliana?

Ama Cindy na Sheila, Zuberi na Rujiana?

Cinderella na Shamila, Aziza na Severina,

Nishauri kwenye jina, Amina ama Asina?

 

Niambieni Rwaida, Rehema ama Tamima,

Epifania na Roda, Sarafina na Salima,

Jessica au Saida, Angelina na Neema,

Nishauri kwenye jina, Malia ama Halima?

 

Nitaje pia Habida, Farashuu na Habiba,

Raya, Nirrah na Ida, Hidaya hata Haiba,

Tumuite Zenaida, Lulu, Rubi ama Huba?

Nishauri kwenye jina, Vumilia ama Huda?

 

Mwisho nafukiza udi, haliudi kwenye kona,

Nakumbuka na Waridi, Fauziya na Zarina,

Vipi Pendo na Zawadi, Khadija pia na Fena?

Nishauri kwenye jina, Sabaha au Fiona?

© 2019 Eric Manyota

‘Kongowea Mshairi’

Nairobi.