Habari Mseto

SHAIRI: Ziko wapi haki za wanahabari?

April 22nd, 2018 1 min read

Na KULEI SEREM

Kitendawili natega, nani atakitegua?
Ng’ombe sasa wanataga, kuku wanajifungua,
Ati mtama namwaga, kinywa ninakipanua,
Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?

Tunazipata habari, tena sana kwa wakati,
Mambo yetu huwa shwari, twazipokea ripoti,
Mwasema ni majeuri, hadi kwenye magazeti,
Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?

Na wale watangazaji, wa redio na runinga,
Wana mufti usemaji, sauti kama za ninga,
Mioyo mwatia maji, mwasema eti waringa,
Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?

Wanayo tele mantiki, lugha wanazisarifu,
Huufanya uhakiki, tena kwa lugha sanifu,
Mbona wananyimwa haki, na kuitwa majisifu?
Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?

Kwa zao zile kamera, twajua wanasiasa,
Wanapoziuza sera, dezo dezo bila pesa,
Wakishazipata kura, huwaacha kwenye visa,
Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?

Ili kupata kiini, cha maswala hudadisi,
Wanabanwa umatini, wakitafuta nafasi,
Wakiwa pao kazini, hunyanyaswa na polisi,
Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?

Ninafikia tama, mkono nawapungia,
Sikizeni ninasema, akilini kupenyea,
Hamna budi kukoma, kule kuwaingilia,

Nauliza ziko wapi, haki za wanahabari?