Habari Mseto

Shakahola: Washtakiwa wa kike kupelekwa kinyozi kukata nywele chafu

February 6th, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

MAHAKAMA Kuu ya Malindi imetoa agizo kwa usimamizi wa magereza wanakozuiliwa washtakiwa wa kike wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya watoto 191, kuwapeleka kwa kinyozi kukata nywele ndefu na chafu.

Akitoa agizo hilo mnamo Jumanne, Jaji Mugure Thande aliamrisha wasimamizi wa gezera la Shimo la Tewa ambako washtakiwa hao wanazuiliwa, kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba wamewapeleka kunyolewa.

Wanawake hao wenye nywele ndefu ni miongozi mwa washukiwa 29 walioshtakiwa pamoja na mhubiri Paul Mackenzie wa kanisa la Good News International.

Kwa mujibu wa nakala ya mashtaka yenye kurasa 298, washtakiwa hao walisababisha vifo vya watoto 191 msituni Shakahola katika Kaunti ya Kilifi katika tarehe tofauti kati ya Januari 2021 na Septemba 2023.

Washtakiwa hao wa kike walipokuwa katika mahakama ya Malindi mnamo Jumanne walionekana kuwa na nywele ndefu.

Baadhi ya mafundisho ya dhehebu la Good News International yalikuwa hayaruhusu wanawake kuwa na nywele ndefu.

Wakati watu walikuwa wakiookolewa katika msitu wa Shakahola wakati wa operesheni ya kuwasaka na kuwaokoa waumini walioanguka kwa mtego wa mafundisho potovu, wanawake wote waliopatikana walikuwa wamenyoa nywele.