Michezo

Shakava afurahia kujitolea kwa wenzake licha ya ratiba ngumu

June 25th, 2018 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Nahodha wa Gor Mahia, Harun Shakava amewapongeza wenzake kwa kustahimili ratiba ngumu inayowakabili msimu huu.

Gor walihifadhi taji la Super Cup na vile vile wanashiriki katika michuano ya kuwania ubingwa wa CAF Confederations Cup, Shield Cup, na mechi za kuwania Ligi Kuu ya Kenya (SportPesa Premier League kwa wakati mmoja.

Kadhalika, mabingwa hao wanajiandaa kushiriki katika michuano ya Kagame Cup nchini Tanzania.

Mechi ya kirafiki dhidi ya Everton nchini Uingereza pia inawasubiri mwezi ujao.

“Kwa hakika, msimu huu tuna mzigo mkubwa kutokana na ratiba inayofuatana kwa karibu. Pamoja na hayo yote, hatuna wakati wa kupumzik, lakini nina hakika tunafaulu,” Shakava alisema jana.,

Nahodha huyo anaamini klabu hiyo iko katika hali nzuri ya kutwaa mataji tofauti kwa wakati mmoja.

“Muelekeo wetu ni mzuri…. tutaendelea kujitahidi kwa sababu hatuwezi kufaulu bila bidii. Umoja lazima uwepo kila wakati kwa ajili ya mafanikio. Tunafanya kazi pamoja kwa maslahi yetu, tunafurahia ushirikiano wetu,” aliongeza.

Gor watacheza na Posta Rangers na baadaye Sony Sugar kabla ya kuondoka kuelekea Dar es Salaam kushiriki michuano ya Kagame Cup.