Michezo

Shakhtar Donetsk wapepeta Basel na kujikatia tiketi ya kuvaana na Inter Milan kwenye nusu-fainali ya Europa League

August 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHAKHTAR Donetsk kutoka Ukraine waliibandua FC Basel ya Uswisi kwenye robo-fainali ya Europa League msimu huu baada ya kuwatandika kwa mabao 4-1 mjini Gelsenkirchen, Ujerumani mnamo Agosti 12, 2020.

Miamba hao wa soka ya Ukraine watapepetana sasa na Inter Milan ya Italia kwenye hatua ya nusu-fainali mnamo Agosti 17, 2020 mjini Dusseldorf. Manchester United na Sevilla kutoka Uhispania watavaana katika nusu-fainali nyingine.

Donetsk walifungua ukurasa wao wa mabao kupitia kwa Junior Moraes katika dakika ya pili kabla ya Taison Freda kufunga la pili kunako dakika ya 22.

Alan Patrick alijaza kimiani goli la tatu la Donetsk kupitia penalti iliyopatikana baada ya Taison kuchezewa visivyo.

Dodo Cordeiro alifunga bao la nne katika dakika 88, sekunde chache kabla ya Basel kufutiwa machozi na Ricky van Wolfswinkel.