Michezo

Shalke na Berlin nguvu sawa

June 7th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI Jonjoe Kenny anayechezea Schalke kwa mkopo kutoka Everton, alipachika wavuni bao muhimu lililowavunia alama moja kutokana na sare ya 1-1 dhidi ya Union Berlin katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Kwingineko, Wolfsburg walisajili ushindi wa 1-0 na kuwaning’iniza Werder Bremen pembamba zaidi kwenye msimamo wa jedwali la Bundesliga.

Bao la Kenny lilikuwa lake la pili katika soka ya Ujerumani tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Union walijiweka uongozini kunako dakika ya 11 kupitia Robert Andrich kabla ya Kenny kusawazisha mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Awali, mvamizi Wout Weghorst wa Wolfsburg alikuwa amevunia waajiri wake alama tatu muhimu kutokana na bao lake la dakika ya 82 dhidi ya Bremen ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya 17 kwa alama 25, tano zaidi kuliko Paderborn wanaovuta mkia.

Bao la Weghorst lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Felix Klau. Goli hilo lilikuwa lake la kwanza baada ya mechi tano za Bundesliga.

Ni pengo la alama sita kwa sasa ndilo linalotamalaki kati ya Bremen na Mainz waliowapepeta Eintracht Frankfurt 2-0 ugenini.

Ushindi kwa Wolfsburg ulipaisha jedwalini hadi nafasi ya sita kwa alama 45, mbili zaidi kuliko Hoffenheim wanaosoma mgongo wao.

Union wanakamata nafasi ya 14 kwa alama 32, sita nyuma ya Schalke ambao wamesajili ushindi mara moja pekee kutokana na jumla ya michuano 13 iliyopita.

Katika mechi nyingine ya Bundesliga, kiungo Anthony Modeste alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Cologne bao kunako dakika ya 85 kabla ya juhudi zake kufutwa na beki Philipp Max aliyewasawazishia Augsburg.

Matumaini ya Bremen kuponea shoka la kuwateremsha daraja mwishoni mwa muhula huu yalididimizwa zaidi mnamo Juni 3, 2020 baada ya kupokezwa kichapo cha 3-0 na Frankfurt ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya 11 kwa alama 35.

Huku Bremen wakikodolewa na hatari ya kuteremshwa daraja kwenye kivumbi cha Bundesliga kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 1981-82, Wolfsburg sasa wanatawaliwa na hamasa ya kumaliza miongoni mwa vikosi sita-bora kileleni mwa jedwali ili kunogesha soka ya bara Ulaya kwa msimu wa pili mfululizo.

Wolfsburg walijibwaga ugani dhidi ya Bremen wakitawaliwa na kiu ya kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa kwa 2-1 na Eintracht Frankfurt mnamo Mei 31, 2020.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Juni 7, 2020):

Bremen 0-1 Wolfsburg

Union Berlin 1-1 Schalke

Augsburg 1-1 Cologne