Shalom Yassets inavyookoa vijana mitaani

Shalom Yassets inavyookoa vijana mitaani

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Shalom Yassets kando na kunoa vipaji vya mchezo wa soka pia inalea washiriki wake kiroho. Ilianzishwa mwaka 1992 chini ya Wakfu wa Shalom katika kumbatio la Padri Renato Kizito wa Koinonia Community.

Ikiwa chini ya makocha, Geoffrey Erambo, George Wafula na Wycliff Juma imejitwika jukumu la kukuza na kulea vipaji vya wanasoka pia kusaidia kwa hali na mali kwa mafaao yanayostahili kimaisha. Kikosi hiki hufanyia mazoezi pia kuandaa mechi za ligi katika uwanja wa Kinyanjui Technical, Riruta Nairobi.

Shalom Yassets ni miongoni mwa vikosi vinavyotifua vumbi kali kwenye mechi za Kundi B kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu. Kocha Geoffrey Erambo anasema wamepania kujituma kwa udi na uvumba ili kujikatia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao.

Kwenye jedwali la mechi za Kundi hilo, Shallom Yassets chini ya nahodha,Ford Ikulwa inashikilia nafasi ya saba kwa kuzoa alama 11, sawa na Kuwinda United baada ya kupiga mechi nane na tisa mtawalia.

KULEA

Licha ya kwamba zipo timu zilizo mbele yao kwenye jedwali ya kipute hicho, kocha huyo anasema ”Baada ya kutazama vijana wangu jinsi wanavyocheza nimegundua wazi kwamba hakuna upinzani mkali mbali wanahitaji kujikaza dimbani ili kutimiza azma yetu muhula huu.”

Shallom Yassets inajivunia kunoa makucha ya wachezaji wachache kama Chris Wekesa (Gor Mahia FC) na Andrew Ongwae (City Stars) ambazo hushiriki Ligi Kuu ya Kenya (BKPL).

Pia yupo Brian Mzee kati ya wengine ambaye huchezea Ligi Ndogo FC. Katika mpango mzima timu hii inatafuta ufadhili zaidi ili kuisongesha mbele na kuanzisha miradi ya kusaidia wachezaji kwa hali na mali kando na kuwaandaa kushiriki ligi za hadhi ya juu nchini.

MATAJI

Viongozi wa timu hii wanaomba vinara wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutafuta wadhamini kuzisaidia klabu za ligi za viwango vya chini maana hujipata njiapanda kugharamia mahitaji yote ikiwamo kulipa marefarii na walinzi wakati wa mechi za ligi. Kwenye juhudi za kukuza wachezaji wake timu hii inajivunia kushinda mataji kadhaa tangia ianzishe.

Baadhi ya mashindano hayo yakiwa: Koinonia Cup (1998 na 2002), K Rep Bank Cup (2002), Don Bosco Cup (2002, 2003, 2004, 2010 na 2012), Dennis Cup (2012) na Amani Onlus Cup (2006).

Pia imeibuka katika nafasi ya pili kwenye mashindano mengine kama Mundial Roma Cup (2004) na Chairman Cup (2011), Jesus Cup(2017/2018) pia mwaka jana walitawazwa wa URBUNU GICUHI Cup mara tatu. Kwenye juhudi za kukata kiu ya soka kwa wachezaji wanaokuja timu hii ina vikosi vya vitengo tofauti kama kwa wasiozidi umri wa miaka 13, 15, 17 na 20.

  • Tags

You can share this post!

Covid: Raia lawamani kwa kupuuza kanuni

Brenda Ochieng anavyotesa katika tasnia ya uigizaji