Shalom Yassets yawatandikia vijana zulia la upenyo

Shalom Yassets yawatandikia vijana zulia la upenyo

Na PATRICK KILAVUKA

NENO Shalom linapotajwa wengi hukumbushwa kuhusu maana ya amani.

Mja huhisi vyema anapoonyesha uanataaluma au kipaji alichoruzukiwa na jalali ili afikie makusudi katika mazingira ya amani. Kauli mbiu hii, ndiyo ilijenga msingi wa timu ya Shalom Yassets ambayo inapatikana uwanja wa Chuo cha Kiufundi cha Kinyanjui, Riruta Satelite kimazoezi na kushiriki michuano ya vipute na ligi.

Timu hii kulingana na Benchi inayoongozwa na mkufunzi Geofrey Erambo, meneja wa timu Wycliff Juma na kapteni Ford Ikulwa, imetuliza wanavipaji vya soka kwa miongo kadhaa na hivyo basi kuwapa jukwaa la kuvikuza kwa njia ya amani.

“Tunaamini amani ni msingi mwema wa kulea kila kitu kwani pasi na amani, mja huwa na mshike mshike wa kimawazo na matokeo ya kuridhisha huwa hayapatikani katika hali ambayo nyongo imevurugwa katika udhibiti. Hali yose ikitokea, timu nyingi zinazoshiriki ligi kuu mbalimbali nchini husambaratika,” wanasema wadau hao ambao wanawajibikia kisima kikuu cha kabumbu ambacho kimekuwa uhai kwa miongo mitatu na kulea takriban vizazi vinne kiamani na kuamini.

Azma ya timu imekuwa tu kukuza na kulea vipawa. Isitoshe, kuwasaidia vijana kwa hali na mali kwa mafaao yanayostahili kimaisha.

Maazimio hayo yamewawezesha wanasoka ambao wamepitia katika timu hii, chini wakfu wa Shalom ambao umo katika kumbatio la Padri Renato Kizito wa Koinonia Community kuona umaana wa kujitahidi maisha na kupiga chenga changamoto za kimaisha.

Kwa sasa, ina wanasoka zaidi ya 40 wa timu ya wakubwa, japo ni kituo pia ambacho kimezingatia kukata kiu ya soka kwa vitengo vya wasiozidi umri wa miaka 13,15, 17 na 20 hemani.

Yassets imewahi kucheza Ligi za hadhi mbalimbali kwa miaka kumi kabla kukumbwa na changamoto za ufadhili zaidi na ikaanza kurudi kujipanga tena kwa kujisajili katika Ligi ya Kanda ya Shirikisho la Soka Kenya, Nairobi West msimu wa 2015-2016. Isitoshe, ilicheza Ligi ya Extreme Sports Super Eight (SPS8), 2017 na kwa sababu ambazo hawangeziepuka, timu haikuendelea kushiriki ligi hiyo.

Mwaka 2017, ilianza kujitanua upya kwenye ligi ya Kaunti Ndogo ya Shirikisho la Kabumbu Kenya, tawi la Nairobi West na kuibuka kileleni. Msimu wa 2018-2019 ilipanda ngazi kushiriki Ligi ya Kaunti ya FKF, tawi hilo na kuibuka ya kwanza pasi na kutokushindwa. Msimu wa 2019-2020 ilibuka ya pili bora nyuma ya South B na kupandishwa ngazi ya Ligi hiyo kushiriki Ligi ya Kanda ya Shirikisho hilo, (NWRL). Hata hivyo msimu wa 2020, ilikuwa imecheza mechi saba kabla ndwele la janga corona kukurupuka na ligi ikasitishwa.

Msimu huu, imeanza kwanza matao zaidi kwa kuicharaza Red Carpet 0-0, kuzabwa na Karura Greens 3-2 na kufuma Kuwinda 1-0 kufikia kuandikwa kwa makala haya.

Katika kuimarisha timu kwa msimu huu, kocha Erambo alisema walisajili wachezaji kama kipa Lawrence Baraza, madifenda Nicholas Maruti na Peter Waweru na kiungo Oscar Afubwa na Emmanuel Mande kukasa nati za safi hizo.

Timu imechipuza pia vipawa vya soka ambavyo vimenadiwa kambi za timu zingine kama straika Brian Mzee na kipa Bruce Omwenga ambao wamo kikosi cha Ligi Ndogo na Kiungo mkabaji ambaye ameyoyomea kisima cha Gor Mahia Youth.

Wachezaji wamefaidika kimaisha kwani wengi wanapata mafunzo ya taaluma za masuala ya biashara, mapishi, mapokezi na hoteli pamoja na ya kijamii katika Taasisi ya Diakonia kwa kugharamiwa karo kia.

Wengine baada ya mafunzo wanaajiriwa na kuendelea kulea talanta zao kambini mwa Yassets.

Mipango ya timu sasa ni kutafuta ufadhili zaidi wa kuisongesha mbele na kuibua miradi ya kuwasaidia wanasoka kwa hali na mali kando na kuiandaa kushiriki Ligi za Taifa haswa kwanzia ligi ya Daraja ya Pili baada ya kupepetana katika Ligi ya Kanda.

Wadau wanaliomba Shirikisho la Kandanda Kenya kujaribu kuzisaidia timu kwani, timu au vilabu vinahangaika zaidi kugharamia matakwa yote ya kimechi yakiwemo mahitaji ya usafiri, kulipa marefa na walinzi ilhali hazina zao zimeinama hali ambayo inayumbisha ustawi wa timu nyingi japo kuna makocha ambao wamejitolea kuvilea vipaji.

  • Tags

You can share this post!

Masoud Juma, Duncao Ochieng’ wachana nyavu katika...

Washukiwa wawili Thika wanaswa na lita 4,000 za pombe haramu