Dondoo

Shambaboi taabani kuiba fegi ya bosi

April 4th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

MATUU, MACHAKOS

POLO aliyeajiriwa kazi ya shamba boi eneo hili alilazimika kupiga nduru baada ya kupapurwa na mdosi wake kwa kuvuta sigara yake.

Inasemekana mdosi aliacha kipande cha sigara mezani naye shamba boi akakichukua na kukiwasha akaanza kupiga pafu.

Haikuwa mara ya kwanza mwenye boma kupoteza sigara zake za bei ghali katika hali isiyoeleweka akiwa nyumbani na siku hiyo aliacha kipande cha sigara maksudi kujua mwizi alikuwa nani.

Kulingana na penyenye, muda mfupi baada ya kuacha sigara hiyo, buda alinusa harufu ya sigara yake ikitoka nyuma ya choo. Alienda kuangalia na kupata shamba boi akiendelea kujitia stimu kwa raha zake.

Alipogundua jamaa alikuwa akivuta sigara yake, alimrukia na kumzaba makofi huku akimlaumu vikali kwa kutomheshimu.

“Mwizi wewe. Ni nani alikupa ruhusa ya kuchukua sigara yangu na kuivuta. Umeniudhi sana na leo nitakufunza adabu ili ujue unapaswa kuniheshimu,” buda alimwambia shamba boi huku akiendelea kumwadhibu.

Jamaa aliomba msamaha lakini mdosi alimpuuza. “Pole mdosi naomba unisamahe. Sio kupenda kwangu ni majaribu tu. Nilihitaji stimu ili nifanye kazi nikiwa nimechangamka,” polo alijitetea.

Baadaye ilibidi jamaa apige nduru kuomba usaidizi alipoona maisha yake yalikuwa hatarini.

“Njooni mnisaidie. Naumizwa na mdosi wangu,” jamaa alilia. Inasemekana watu waliitikia wito huo na kwenda kujua kilichokuwa kikijiri kwa buda.

Majirani walipigwa na mshangao kupata mdosi akimkaba jamaa koo akimlaumu kwa kuvuta sigara yake. Hata hivyo walimsihi mzee kutuliza hasira zake na kumwacha shamba boi.

Hatimaye mzee alimpiga kalamu shamba boi huyo na kumuonya kutotia guu lake kwake.