Habari Mseto

SHAMBULIO: Majonzi shabiki maarufu kufariki siku yake ya kuzaliwa

January 16th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

JAMII ya soka inaomboleza baada ya shabiki maarufu kwa jina James Oduor, anayetambulika kama ‘Odu Cobra’ kuangamia katika shambulio la hoteli ya Dusit D2, 14 Riverside Drive, katika siku ya kuzaliwa kwake.

Bw Oduor alikuwa mpenzi mkubwa wa kandanda na pia mchezaji ambaye alienziwa na wengi.

Wakati wa uvamizi huo, alizungumza kupitia mitandao ya kijamii, akieleza namna alivyohofia na kuwa hakufahamu kilichokuwa kikiendelea.

Cha kushangaza ni kuwa siku maiti yake ilipopatikana, Jumatano, ndiyo siku aliyotarajia kusherehea kuzaliwa kwake.

Wanahabari tajika Larry Madowo na Carol Radull ni baadhi ya watu waliotuma rambi rambi zao kwa familia ya Bw Oduor.

“Rafiki yangu wa tangu chuo kikuu aliuawa siku moja kabla ya kusherehekea kuzaliwa kwake. Alikuwa ndiye mtu mcheshi na mkarimu sana ambaye nimewahi kukutana naye,” akasema Bw Madowo.

“Ndio, sote tulikuwa marafiki na Odu. Nguvu katika kandanda ya Kenya. Uchungu sana. Naombea bintiye mchanga na familia nyingi ambazo zimeadhirika na mkasa huu,” Bi Radull akasema.

Bw Oduor alikuwa akifahamisha ulimwengu namna matukio yalikuwa, japo hakujaaliwa kupona.

Saa tisa na nusu Jumanne, aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter “Nini kinaendelea eneo la 14 Riverside. Tumezuiliwa katika majengo yetu.”

“Milio ya bunduki na milipuko isiyoisha,” akaandika dakika moja baadaye.

“Waaaah, nini kinaendelea 14 Riverside marafiki? Kuna habari zozote huko nje?” akaandika dakika tatu baadaye.

Cobra alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya LG iliyo na makao eneo la 14 Riverside.

Mwenyekiti wa FKF Nick Mwendwa aidha aliongoza wapenzi wa soka kumwomboleza shujaa huyo, akisema “Safiri salama rafiki yangu. Mapenzi yako yataishi katika soka. Ulifanya kazi yako. Tutafanya yetu na kukukumbuka,” Bw Mwendwa akachapisha katika Twitter.

Wapenzi zaidi na mashabiki wa soka walilia kwenye mitandao ya kijamii, wote wakiomboleza kufariki kwa mtu waliyemwona shujaa na nguvu ya msukumo wakati wa burudani za kandanda.