Habari

SHAMBULIO: New York Times yakumbana na ghadhabu za Wakenya mitandaoni

January 16th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU 

SHIRIKA la habari la Marekani, New York Times limekashifiwa baada ya kuchapisha picha za wafu, kufuatia vamizi lililotekelezwa katika hoteli ya Dusit, mtaa wa Riverside Jijini Nairobi Jumanne. 

New York Times ilichapisha picha tofauti za watu waliofariki kwenye mitandao kupitia Getty Images na The Associated Press, zikitoka kwa tawi la shirika hilo la habari la Afrika Mashariki.

Lakini hali hiyo iliwagadhabisha sana watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao walilaani ukosefu wa maadili wa shirika la kimataifa la habari, na kuwakashifu.

Aliyekuwa mhariri wa NTV Wallace Kantai na mtangazaji wa kituo hicho wa zamani Larry Madowo walijiunga na Wakenya na watu wengine kote kukashifu picha na chapisho la kampuni hiyo.

Waliwakosoa mwandishi na shirika hilo kwa kuchapisha picha za wafu.  Mwandishi de Freytas- Tamura, hata hivyo baadaye aliomba msamaha kwani picha zilitumika katika hadithi yake, akisema “kwa niaba ya New York Times naomba msamaha kwa kughadhabisha na kuhuzunisha watu kuhusiana na picha ambazo zimechapishwa kupitia habari zetu. Asanteni,” akasema Jumanne, Januari 15.

Akaunti ya picha ya shirika hilo kwenye Twitter aidha imepigwa marufuku kwa kuchapisha picha zisizofaa.

Wakenya walishangaa kwa nini shirika hilo kwa kawaida halichapishi picha za wafu wakati wa mashambulizi yanayosababisha vifo vingi katika shule za Amerika na mkahawa ya mataifa yaliyoendelea.

“Mbona ni rahisi kwao kuchapisha picha za wafu katika shambulio linalofanyika katika taifa la Afrika?” Mkenya mmoja alishangaa kwenye Facebook.

Ikulu ya Nairobi imewashauri watu kutosambaza picha za kuogofya kutoka za vamizi la Riverside.  Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet aidha aliwataka Wakenya kutotumia picha za zamani za mavamizi mengine, mkwani itakuwa sawa na kusherehekea.