Habari Mseto

SHAMBULIO: Ni miaka 3 kamili tangu Al Shabaab waue wanajeshi El Adde

January 16th, 2019 1 min read

Na WYCLIFFE MUIA

SHAMBULIO la Jumanne katika hoteli ya Dusit eneo la Riverside jijini Nairobi lilitokea miaka mitatu kamili baada ya shambulizi la al Shabaab katika kambi ya jeshi la KDF ya El Adde nchini Somalia.

Shambulio hilo lililotajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kukumba maafisa wa KDF wanaohudumu Somalia tangu Oktoba 16, 2011 wakipambana na magaidi wa al Shabaab, liliacha maswali mengi ambayo bado hayajajibiwa na serikali ya Kenya.

Kufikia sasa, serikali haijawahi kutoa idadi kamili ya maafisa wa KDF waliouawa.

Siku chache baada ya shambulio hilo, Mkuu wa Majeshi nchini Samson Mwathethe aliahidi kutoa habari kamili kuhusu kilichofanyika siku hiyo.

Jeshi la Kenya lilibuni jopo la kuchunguza kwa nini idadi ya maafisa waliouawa katika kisa hicho ilikuwa ya juu mno, na mpaka leo ripoti hiyo haijawahi kutolewa kwa Wakenya.

Tangu wakati huo, Taifa Leo imeorodhesha mazishi 40 ya maafisa wa KDF ambao walizikwa katika maeneo mbalimbali.

Baadhi ya familia za wanajeshi waliotoweka baada ya kisa hicho bado zinangoja majibu kutoka kwa serikali huku Jenerali Mwathethe akisema baadhi ya miili iliharibiwa kiasi cha kutotambulika.

Magaidi wa Al shaabab walidai kuwaua zaidi ya maafisa 100.