Michezo

Shane Long kusakatia S'oton hadi afikishe miaka 35

June 7th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI wa Southampton, Shane Long, 33, ametia saini mkataba mpya wa miaka miwili katika makubaliano ambayo kwa sasa yatamdumisha uwanjani St Mary’s hadi mwishoni mwa msimu wa 2021-22.

Nyota huyo mzawa wa Jamhuri ya Ireland aliingia katika sajili rasmi ya Southampton mnamo 2014 baada ya kuagana na Hull City.

Long anajivunia kufungia Southampton mabao 35 na mchuano wake wa 200 ndani ya jezi za kikosi hicho ulikuwa ule uliowashuhudia wakipokea kichapo cha 1-0 kutoka kwa Newcastle United mnamo Machi 7, 2020.

“Naridhishwa na namna kikosi kinavyoendeshwa na tumejiwekea malengo mapya ya kufikia chini ya kipindi cha miaka miwili ijayo. Tumepania kusonga juu zaidi kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na itakuwa tija na fahari tele kuwa sehemu ya ufanisi huo,” akasema Long.