Habari Mseto

SHANGAZI: Akiwa mbali natamani burudani, akikaribia simtaki

January 24th, 2019 2 min read

NA SHANGAZI SIZARINA

Hujambo shangazi? Mimi nimeolewa na nina shida kidogo. Nimekuwa nikipandwa na hamu ya kurusha roho na mume wangu anapokuwa mbali lakini hatimaye nikiwa karibu naye hisia hizo zinatoweka. Nishauri.

Kupitia SMS

Shughuli hiyo hufaulu kutokana na ushirikiano kati ya wawili. Ni muhimu uwe ukimfahamisha mwenzako wakati hisia hizo zinapopanda hata kama yuko mbali ili kuchochea mawazo yako na yake. Hatimaye mkikutana kila mmoja atakuwa tayari kwa mwenzake na mambo yatakuwa sawa.

Nahisi kijana hanitaki

Kwako shangazi. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa 30 na nimevutiwa kimapenzi na mwanamume wa miaka 26. Tatizo ni kwamba nahisi kuwa yeye hanipendi. Nifanyeje? Kupitia SMS

Kama umeona dalili kuwa mwanamume huyo hakutaki hakuna unaloweza kufanya kwa sababu huwezi kumlazimisha kukupenda. Achana naye utafute mwingine.

Husema kwa maneno wala si kwa matendo

Kwako shangazi. Kuna msichana ambaye tumejuana majuzi tu na ninampenda kwa dhati. Yeye pia anasema ananipenda lakini nikimwangalia naona ni kama hana hisia kwangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huwezi kupima hisia za mtu kwako kwa kutumia macho wala hakuna kifaa cha kupimia hisia. Kama amekwambia mwenyewe kuwa anakupenda huna sababu ya kumshuku. Utaweza tu kujua ukweli kupitia vitendo vyake jinsi uhusiano wenu unavyoendelea kukomaa.

Mimba si yangu, nalia

Kwako shangazi. Mimi na mpenzi wangu tunaishi miji tofauti. Mpenzi wangu amekuwa akiniambia ananipenda sana lakini nimeshangaa kugundua kuwa ana mimba ambayo kwa hakika si yangu na bado anasisitiza kuwa ananipenda. Nimechanganyikiwa, nishauri.

Kupitia SMS

Hali kwamba mpenzi wako amepata mimba na una hakika si yako ni thibitisho kwamba si mwaminifu kwako na ana uhusiano mwingine. Huo ni usaliti wa kimapenzi na ningekuwa wewe ningemuachia huyo aliyempa mimba.

Baada ya kuwekeza sana kwake kanisaliti

Shangazi kwanza nashukuru kwa ushauri wako mzuri. Pili, kuna msichana mpenzi wangu tuliyekuwa tumepanga kuaona hata nikamwekea biashara ya pesa nyingi. Sasa nimeshangaa kugundua kuwa ana uhusiano na mtu mwingine. Nifanyeje? Kupitia SMS

Mapenzi hutokana na hiari, huwezi kulazimisha mtu akupende. Kama msichana huyo ameamua kupenda mtu mwingine hiyo ni haki yake. Hata hivyo, itabidi mzungumze ili urudishe pesa zako ulizotumia kumwekea biashara hiyo kwani ninaamini ulifanya hivyo ukiamini kuwa hatimaye atakuwa mke wako.

Nashindwa kumsahau

Kwako shangazi. Kuna mwanamke tuliyekuwa wapenzi lakini uhusiano wetu ukavunjika karibu mwaka mmoja uliopita. Tatizo ni kuwa nimeshindwa kabisa kumsahau. Nifanyeje kumuondoa katika mawazo na moyo wangu? Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa uhusiano kuvunjika ingawa mara nyingi huacha mhusika au wahusika wote na majeraha moyoni. Hatua ya kwanza ya kuondoa mawazo kuhusu mpenzi mliyeachana ni kukubali kuwa uhusiano umevujika. Pili, ni kuchukua hatua ya kutafuta uhusiano mpya.

Najuta kwa kumkosea

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na kijana fulani. Nilipata picha zake akiwa na mwanamke mwingine nikazichoma na alipojua tukakosana. Nampenda sana na natamani turudiane. Nishauri.

Kupitia SMS

Ulifanya makosa kuchoma picha za mwenzako hata kama alikuwa amepigwa akiwa na mwanamke mwingine. Hata kama alikuwa mpenzi wake na wakaachana, picha haziwezi kuathiri uhusiano wenu. Muombe msamaha uone kama atakubali kukusamehe.

Simpendi tena mume

Shangazi mimi niliolewa na mume niliyempenda sana lakini kwa sasa mapenzi yangu kwake yametoweka kwa sababu ya maudhi ya kila mara. Kuna mwanamume mwingine mbaye amenitongoza na ameteka moyo wangu nahisi kama ameganda humo. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kwanza, kumbuka kuwa umeolewa kwa hivyo huwezi kuamka siku moja na kuamua kuondoka ukaolewe na mtu mwingine. Kama kuna mambo anayokufanyia mume wako ambayo unahisi huwezi kuendelea kuvumilia ni muhimu umwelezee wazi ili kama ni kutengana iwe ni kupitia maelewano.