Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Adai alitenda dhambi kuonja asali, ataka tuachane

June 5th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

MAMBO shangazi? Juzi nilimpata mwanamume mpenzi wangu amekasirika sana na nilipomuuliza sababu akaniambia eti alifanya dhambi kwa kushiriki mahaba na mimi na sasa anataka tuachane. Ninampenda sana na uamuzi wake huo unanikosesha usingizi. Tafadhali naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa mwanaume huyo hakuwa na haja na uhusiano bali alitaka tu kulamba asali na baada ya kuipata ameamua kutumia hicho kuwa kisingizio cha kukutema. Kama anahisi alifanya dhambi, anafaa kutubu dhambi zake kisha muendelee na uhusiano wenu na kuepuka tendo la ndoa hadi mtakapooana. Tumia kauli hizi kushauriana naye na akikataa ujue hana haja nawe, ameshapata alichokuwa akitaka.

 

Nahisi anapendelea zaidi ya mke wa pili

Hujambo shangazi? Nimeolewa na mume wangu pia ana mke wa pili anayefanya kazi mjini. Tatizo ni kuwa mume wangu anapomtembelea mke-mwenza huwa hataki kabisa simu zangu, lakini akiwa kwangu huwa anawasiliana naye. Tabia yake hiyo inanichukiza kwani nahisi kuwa ananibagua. Nishauri.

Kupitia SMS

Ndoa zina changamoto nyingi hasa zinazohusisha wanawake zaidi ya mmoja. Ninakubaliana nawe kuwa kwa namna fulani kitendo cha mume wako kinaonyesha aina ya ubaguzi kwani anafaa kuzingatia usawa kwenu nyote. Badala ya kunyamaza na kulalamika kimyakimya, ni muhimu ushauriane naye kuhusu suala hilo ajue unavyohisi ili ajirekebishe.

 

Nilitafutia mpenzi kazi sasa anidharau

Shangazi hujambo? Nimekuwa na mpenzi kwa muda mfupi. Tulipokutana hakuwa na kazi na nilijitahidi nikamtafutia. Lakini punde tu alipoingia kazini msichana alianza kunidharau. Juzi alinipigia simu akaniambia hataki mambo yangu. Nafikiria kulipiza kisasi kwa kumtoa kwa hiyo kazi. Nishauri.

Kupitia SMS

Inaonekana msichana huyo alitaka kukutumia kupata kazi na ndiyo maana ameamua kukutema kwani ametimiza lengo lake. Ushauri wangu ni kuwa usilipize kisasi. Ulimfaa kwa haja yake na ingawa shukrani yake imegeuka mateke, Mungu atakulipa kwa wema wako.

 

Si kawaida mpenzi kuninyamazia bure

Hujambo shangazi? Tafadhali nahitaji ushauri wako. Miaka mitatu iliyopita nilikutana na mwanamume fulani na tukapendana. Nilikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu naye alikuwa mfanyakazi wa kampuni fulani maarufu. Ingawa alibanwa sana na kazi yake, alitenga wakati wetu kuwa pamoja. Sielewi imekuwaje kwani ni wiki mbili sasa hatujaonana wala kuwasiliana. Nimemtumia SMS lakini hajibu. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Hiyo ni mojawapo ya changamoto za mahusiano. Inakuwa hali ya kuvunja moyo sana mtu anapoungama mapenzi yake kwako na ukishampa moyo wako hatimaye anakuacha bila sababu. Sisemi kuwa mpenzi wako amekuacha kwani mwenyewe hajakwambia hivyo, labda ana sababu nzuri ya kutowasiliana nawe kwa wiki hizo mbili. Ni vyema umtafute muonane ana kwa ana akwambie sababu. Ikitokea kwamba ameamua hataki kuendelea na uhusiano, itabidi ukubali uamuzi wake kwa sababu huwezi kumlazimisha.

 

Mbona anisukuma nijenge karibu kwao?

Shikamoo shangazi! Nina uhusiano na mwanamke mwenye umri wa miaka 40 nami nina miaka 28. Ninaamini anaweza kuwa mke mzuri lakini nahisi tofauti ya umri kati yetu ni kubwa. Pili, ananisukuma ninunue shamba karibu na nyumbani kwao tujenge ilhali kwetu nina shamba na tayari nimejenga. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sharti la mwanamke huyo kwamba ni lazima muishi karibu na wazazi wake halina msingi. Wewe ndiye unayemuoa kwa hivyo unafaa kuamua kuhusu mahali mnapofaa kuishi. Kuhusu umri, nimesema mara kadhaa hapa kuwa hauwezi kuwa kikwazo katika ndoa bora tu kuna upendo na maelewano kati ya wahusika.