Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Alikimbilia mwanamume mwingine, sasa amerudi

August 2nd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nilikuwa na mpenzi na tukazaa mtoto pamoja. Lakini aliniacha akaolewa na mwanamume mwingine. Sasa wameachana na amerudi kwangu akitaka nimtambue kama mke wangu. Mimi simpendi tena wala simtaki katika maisha yangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mwanamke huyo hawezi kurudi kwako kwa lazima hata kama mlizaa pamoja. Uhusiano wenu ulimalizika pale alipokuacha na kuolewa na mwanamume mwingine. Isitoshe, mlipopata mtoto huyo hakuwa mke wako bali mpenzi tu.

 

Jirani ana mke na bado ananiandama

Vipi shangazi? Mimi ni msichana mwanafunzi wa shule ya upili na nina umri wa miaka 19. Kuna mwanamume jirani yetu ambaye anataka tuwe na uhusiano wa kimapenzi ilhali ameoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Tunaishi katika jamii iliyojaa walaghai wa kimapenzi, wanawake kwa wanaume. Mwanamume huyo ni mmoja wao na nakuonya kuwa utakutana na wengine. Hata hivyo, hakuna anayeweza kukulazimisha kuingia katika uhusiano naye. Wewe ni mwanafunzi na kilicho muhimu zaidi kwako sasa ni masomo. Muepuke kabisa mwanamume huyo na wengine wa sampuli hiyo.

 

Wazazi wangu hawamtaki kabisa

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 22 na nina mpenzi ninayempenda sana na tumepata mtoto pamoja. Yeye pia ananipenda sana. Tatizo ni kwamba wazazi wangu hawamtaki. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ndoa ni chaguo na mtu binafsi na kamwe wazazi hawana haki ya kuingilia kwa jinsi yoyote ile. Kama mwanamume huyo ndiye anayeridhisha moyo wako, usikubali kabisa kutenganishwa naye. Isitoshe, tayari mmepata mtoto pamoja na hiyo ni hatua kubwa katika uhusiano wenu.

 

Wa zamani anaamini mtoto ni wake lakini…

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 32 na nimeolewa. Kabla sijaolewa, nilikuwa na mpenzi niliyempenda sana. Alitamani sana nimpe mtoto na tulijaribu mara kadhaa tukashindwa. Nilishikana na mwanamume mwingine wa pembeni ambaye alinipa mimba na hatimaye akanioa. Aliyekuwa mpenzi wangu anaamini mtoto huyo ni wake na sasa anataka kumchukua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mpenzi wako huyo wa zamani ataendelea kuamini kuwa mtoto huyo ni wake kwa sababu hivyo ndivyo ulivyomwambia. Kama unataka kumaliza mvutano kati yenu kuhusu mtoto huyo, mwambie ukweli. Na iwapo haamini, mwambie afanyiwe ukaguzi wa kitaalamu ili ajue ukweli huo, kwamba mtoto si wake.

 

Nashuku sana mume ameanza kuzurura nje

Shangazi pokea salamu zangu za dhati. Nimeolewa kwa miaka mitatu na nina watoto wawili. Mume wangu amekuwa mzuri kwa wakati wote huo hadi siku za hivi majuzi ambapo naona tabia yake imebadilika. Nimeanza kushuku kwamba anatembea nje na mawazo hayo yananinyima raha maishani. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, unamshuku tu mume wako wala huna ushahidi kuhusu jambo hilo. Kwa sababu hiyo, sielewi ni kwa nini unahuzunika bure. Pengine unavyomdhania sivyo. Jaribu kuchunguza ujue ukweli. Na kama kweli anakuchezea, basi jiondokee ukajitafutie maisha badala ya kuishi na mtu asiye mwaminifu.

 

Nilivutiwa kwake siku ya kwanza, shida ni naambiwa ni jambazi

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke tuliyekutana majuzi katika maskani ya burudani na tukapendana. Tumekuwa pamoja kwa miezi miwili tu na amenivutia kwa maumbile na pia tabia yake. Ajabu ni kuwa nimepata fununu kuwa ni mwanachama wa genge hatari la majambazi. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa huwezi kuamini mara moja uliyoambiwa kumhusu, ushauri wangu ni kuwa uchukulie uhusiano huo kwa tahadhari huku ukichunguza mienendo yake. Kama uliyoambiwa ni kweli utajua na ukithibitisha hutakuwa na budi kumuondokea.