Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Aliniacha baada ya kunitusi, anataka turudiane

March 5th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nilikuwa na mpenzi lakini tulikosana miezi miwili iliyopita alipokuja nyumbani kwangu akiwa mlevi. Alizua ugomvi na kunitusi vibaya kwa madai eti nina mpenzi mwingine wa pembeni. Akiondoka aliniambia uhusiano wetu umekwisha na kwamba nimsahau kabisa. Katika wiki moja iliyopita, amekuwa akinipigia simu karibu kila siku akiomba nimsamehe kisha turudiane. Bado nampenda, lakini kufikia sasa sijajua kilichomfanya aniambie mambo aliyoniambia kabla ya kutoweka kwa muda wote huo. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Binadamu hukosea maishani na mara nyingi matokeo yake huwa majuto. Hali kwamba mpenzi wako anakulilia akitaka umrudie licha ya kutangaza mwisho wa uhusiano wenu, ni ishara kuwa anajuta kwa kitendo na maneno yake. Inawezekana kuwa yote hayo yalitokana na ulevi. Ushauri wangu ni kwamba umpe nafasi nyingine. Hata hivyo, ni muhimu kwanza akuhakikishie kuwa hatarudia.

 

Mamake alinikemea

Shikamoo shangazi. Nimependana na msichana tunayesoma pamoja shule ya upili. Juzi nilikutana na mama yake akanikemea vikali akisema ninamharibu binti yake na kunitaka niachane naye mara moja. Nampenda sana msichana huyo na sijui nitafanya nini. Ninaomba ushauri.

Kupitia SMS

Sababu ya mama ya msichana huyo kukukemea ni kwamba unampotosha binti yake kwa kumhusisha na mapenzi ya upuuzi ilhali nyinyi bado ni wanafunzi. Wazazi wako pia wanagharamia masomo yako wakiamini unasoma na huku wewe umeshika mengine. Achana na mtoto wa wenyewe na uzingatie masomo yako.

 

Aliacha mkewe ili tuwe wapenzi

Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka miaka 24 na sijaolewa, ingawa kuna wanaume wengi ambao hudondokwa na mate wakioniona kwa sababu ya umbo langu la kuvutia. Mpenzi wangu wa sasa ni mwanamume aliyekuwa na familia lakini akamuacha mke wake kwa ajili yangu. Juzi mke wake alinitumia SMS kunitishia maisha kwa akidai nimempokonya mume. Nampenda sana mwanamume huyo na sidhani ninaweza kumuacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni haki yako kuchagua mwanamume unayempenda miongoni mwa wote wanaodondokwa na mate wakikuona. Hata hivyo, nakushauri uachane na wanaume walio na familia na kuheshimu ndoa zao. Pili, usijitape eti unawazuzua wanaume kwa urembo wako. Kuna warembo zaidi yako na wengine wanaendelea kuzaliwa. Anayekufuata leo kwa sababu ya urembo wako, kesho atakuacha amfuate mwingine mrembo zaidi yako. Tafakari hayo na ufanye uamuzi wa busara.

 

Nimekosa mpenzi kwa kuwa naogopa wanaume

Vipi Shangazi? Nina shida ambayo inahitaji msaada wako. Nina umri wa miaka 22 na sijawahi kuwa na mpenzi. Natamani sana kuwa na naye lakini huwa naogopa kuzungumza na wanaume. Nimejaribu sana kumaliza hali hiyo lakini nimeshindwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Hali hiyo isikutie hofu sana kwa sababu inatokana na maumbile. Sisi binadamu tumeumbwa kila mmoja kwa namna tofauti. Hata hivyo, maumbile hubadilika jinsi mtu anavyokuwa. Jaribu uwezavyo kutangamana na wanaume na hatimaye woga wa kuzungumza nao utakutoka.

 

Mke ameninyima haki yangu kama mume wake

Shangazi mimi nimeoa na huu ni mwaka wa pili tukiishi pamoja na mke wangu. Tatizo ni kuwa ameninyima kabisa haki yangu ya chumbani. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini umevumilia kunyimwa haki yako ya ndoa kwa miaka miwili bila kuchukua hatua yoyote na badala yake unalalamika tu. Kama hana sababu nzuri ya kukunyima tendo la ndoa, sijui unaendelea kuishi naye kama nani. Utajua mwenyewe la kufanya.