Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Aliniambia ni mimi tu lakini nilipata nguo za mwanamke kwake

November 14th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 28 na nina uhusiano na mwanamume mwenye umri wa miaka 34. Juzi nilimtembelea nyumbani kwake nikapata nguo za mwanamke mwingine. Nilishangaa sana kwa sababu amekuwa akiniambia hana mwingine isipokuwa tu mimi. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Hiyo ni ishara kamili kuwa mwanamume huyo ana uhusiano na mwanamke mwingine ama hata wanawake kadhaa na amekuwa akikuhadaa kuwa ni wewe tu. Jambo pekee la kufanya ni kuachana naye la sivyo ataendelea kukuumiza bure moyoni kwa tabia yake hiyo.

 

Aliahidi kunionjesha asali lakini ameishia kupatia dume lingine

Kwako shangazi. Nimekuwa katika uhusiano na msichana fulani mwanafunzi wa shule ya upili na alikuwa ameniahidi kuwa nitaonja asali akikiashule. Alimaliza shule mwaka uliopita na juzi nilimfumania peupe akiwa na jamaa mwingine nyumbani kwake. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inawezekana kwamba msichana huyo amekuwa na uhusiano halisi wa kimapenzi na mwanamume huyo na amekuwa akikuhadaa kwa muda wote huo. Huna sababu ya kuendelea kuhangaisha moyo wako kwa ajili yake kwa sababu tayari umejua kuwa si mtu wa kuaminika.

 

Tayari nimeshamsahau

Kwako shangazi. Nilikuwa na mpenzi na tukaachana. Hatujawasiliana kwa muda mrefu na sasa amekuwa akinipigia simu akitaka tukutane. Hata hivyo, moyo wangu ushatoka kwake kutokana na dharau aliyonionyesha kabla na baada ya kuachana. Tafadhali naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Wewe ndiye unayejua masaibu uliyopitia mikononi mwa huyo aliyekuwa mpenzi wako. Sijui amefikiria nini baada ya muda mrefu tangu mlipoachana hivi kwamba anataka mrudiane. Iwapo unasema moyo wako umeshatoka kwake, basi huna sababu ya kumpa tena nafasi katika maisha yako. Mwambie wazi kwamba haiwezekani.

 

Aliyeniumiza moyo asema sasa yuko tayari kuuponya

Hujambo shangazi? Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi kwa mwaka mmoja lakini akaniacha bila sababu. Kitendo chake hicho kilinifanya niwachukie wanaume wote na kuamua kuwa hata sitawahi kuolewa. Sasa mwanamume huyo anataka turudiane. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, ninahisi kuwa ulimpenda kwa dhati mwanamume huyo na uamuzi wake wa kukuacha bila sababu ulikuvunja moyo sana. Hata hivyo, utakosea kuwachukia wanaume wote eti kwa sababu mmoja wao alikukosea. Shughuli ya kumtafuta mwenza wa maisha si rahisi na inahitaji subira kwa sababu kila mtu ana kasoro zake. Hata kama hutaweza kumsamehe ili mrudiane, nakushauri ufungue moyo wako ili kutoa nafasi kwa mwanamume mwingine yeyote anayeweza kuthamini penzi lako.

 

Nampenda lakini twakosana kila siku

Hujambo shangazi? Tafadhali nina swali kwako. Nina umri wa miaka 21 na nina mpenzi ambaye nampenda sana. Tatizo ni kwamba tumekuwa tukikosana karibu kila siku. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea wewe na mpenzi wako mmekuwa mkikosana kuhusu mambo gani. Kama kweli mnapendana, ni vyema mketi chini mshauriane kuhusu mambo yanayowafanya mkosane ili muone jinsi ya kuyaepuka.

 

Penzi letu lipo kwenye simu tu, nikimwambia tuonane adai yuko bize

Vipi shangazi? Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye nampenda kwa dhati. Ajabu ni kwamba tumekuwa tukiwasiliana kwa simu tu. Nimekuwa nikitaka tuonane lakini kila nikimuuliza huniambia ana shughuli nyingi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sijawahi kusikia kuhusu uhusiano wa kimapenzi ambao unaendeshwa kupitia kwa simu bila ya wapendanao kuonana. Haiwezekani kwamba huyo mpenzi wako huwa na shughuli mchana na usiku hivi kwamba hana wakati wa kuonana nawe. Inawezekana kwamba moyo wake hauko kwako na hataki kukwambia. Chunguza ili ujue ukweli.