Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Alinihepa lakini moyo ungali kwake, nifanyeje?

September 10th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 28. Kuna msichana tuliyependana sana tukiwa shuleni na nilikuwa nimeamua kuwa ndiye nitaoa. Nilijizuia kabisa kumuomba asali kwa sababu sikutaka kumharibia masomo yake. Isitoshe, nilimsaidia kwa hali na mali tukiwa shuleni nikiamini kuwa mapenzi yake kwangu yalikuwa ya dhati, lakini tulipokamilisha elimu shuleni alinihepa. Ukweli ni kuwa moyo wangu bado umekwama kwake na sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi kati ya vijana mara nyingi huwa hayadumu kwa kuwa wahusika huwa hawaelewi wala kumaanisha wanayosema. Hiyo ndiyo sababu yako kumkosa mpenzi wako kwani mlipomaliza shule alikuwa amekomaa kiasi cha kuelewa anachotaka maishani. Inaonekana aligundua kuwa hakupendi na ndiyo maana alikutoroka. Acha kuhangaisha moyo wako bure. Kubali ukweli kuwa msichana huyo hakutaki na utafute mwingine.

 

Nina mume lakini penzi la pembeni limekuwa tamu mno!

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 30 na nimeolewa. Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani ambaye pia ana familia ingawa bado hajaonja asali kwa mwaka mmoja ambao tumekuwa pamoja. Lakini penzi lake limekuwa tamu sana na sidhani nitaweza kujizuia tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Siwezi kuunga mkono uhusiano kama huo. Sijui wewe na huyo mwanamume mnatafuta nini ilhali kila mmoja wenu ana familia. Hiyo yenu ni tamaa tu wala si mapenzi. Kama kweli mnapendana, kwa nini msivunje ndoa zenu kisha muoane? Siku mume wako au mke wake atakapogundua utajipata kwenye balaa.

 

Kipusa niliyezaa naye ameniletea balaa

Hujambo shangazi? Nimeoa na nimeishi katika ndoa na mke wangu kwa miaka miwili sasa. Kuna msichana niliyempa mtoto tukisoma shule ya upili na sasa ameamua kunivunjia ndoa akitaka nimuoe kwa lazima. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ndoa si jambo la lazima bali ni hiari ya wahusika. Ukweli ni kwamba huwezi kumuoa msichana huyo kwa sababu tayari una mke na ni muhimu umwambie hivyo. Hata hivyo, huwezi kumpuuza kabisa kwa sababu ni mama ya mtoto wako kwa hivyo itabidi uwajibike katika kugharamia mahitaji ya mtoto wenu.

 

Mke amezidi jamani na kunishuku

Shangazi natumai wewe ni mzima. Mimi nina mke ambaye tumeishi pamoja kwa miaka mitatu sasa. Ninampenda sana lakini tatizo ni kwamba anashuku kuwa mimi si mwaminifu kwake. Kila nikipigiwa simu na mwanamke huwa anazua ugomvi nyumbani akisema nina mpango wa kando. Kusema kweli mimi sina uhusiano nje ya ndoa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Tatizo la mke wako ni wivu tu kwa sababu hana ushahidi wowote kuhusu madai yake. Hali yake hiyo inaeleweka kwani ndoa yenu bado ni changa na pia ni ishara kuwa anakupenda kwa dhati. Kama unataka kumuondolea shaka, kuwa ukimwelezea ni kina nani wanaokupigia simu na kuhusu nini. Pili, weka wazi simu yako kwake ili akitaka kuikagua afanye hivyo ndipo athibitishe kuwa huna siri yoyote. Ni kwa njia hiyo tu ambapo ataweza kukuamini na kuondoa wasiwasi.

 

Sitaki kumuonjesha asali hadi nikamilishe masomo yangu

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nina kijana mpenzi wangu. Tunapendana sana na ninaamini atakuwa mwenzangu baadaye maishani. Sasa anataka kuonja asali lakini mimi sitaki nataka kwanza nimalize shule. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nakuonya kuwa mshika mawili moja humponyoka. Wewe ni mwanafunzi na masomo ndiyo kitu muhimu zaidi kwako kwa sasa. Kama unajali masomo yako, weka kando suala ma mapenzi hadi utakapomaliza shule. Iwapo kweli kijana huyo anakupenda kama unavyodai, mwambie asubiri hadi wakati huo.