Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Alinishangaza majuzi kuniambia eti mtoto si wangu!

April 26th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nilikuwa na mpenzi na akapata mtoto tukiwa pamoja. Niliamini mtoto alikuwa wangu na nilikubali jukumu la kugharamia malezi yake. Tulitofautiana na mpenzi wangu miezi miwili iliyopita na tukaamua kuachana. Nilishangaa nilipompigia simu juzi kumwambia nataka kumuona mtoto akaniambia huyo si mtoto wangu wala sina haki ya kumuona. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo mtoto huyo ni wako kumzaa, basi una haki ya kumuona, bora tu mama yake hajaolewa na mwanamume mwingine. Hata hivyo, huenda mama yake anajua anachosema kwani inasemekana kuwa baba ya mtoto amjuaye ni mama. Jinsi pekee ya kujua ukweli ni kupitia ukaguzi wa kitaalamu hospitalini. Ukiweza, fuata njia hiyo ili kumaliza mvutano huo.

 

Ninamshuku huwa ana mpango wa  kando kazini kwake

Nina mume na tumejaliwa watoto wawili. Mimi sina kazi ya kuajiriwa, bali huwa ninahudumia familia yangu. Nampenda sana mume wangu lakini ninashuku kuwa anatembea na mwanamke fulani wanayefanya kazi pamoja. Mawazo hayo yananinyima raha maishani. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo ni kumshuku tu mume wako na huna ushahidi, sielewi ni kwa nini unahuzunika bure. Pengine unavyomdhania sivyo. Jaribu kuchunguza ujue ukweli. Na kama kweli anakuchezea, ni heri uondoke ukajitafutie maisha badala ya kuishi na huzuni.

 

Mpenzi amenisaliti na bado anadai anipenda

Nina mpenzi ambaye nimempa moyo wangu wote kwa miaka mitatu sasa. Hata hivyo, amesaliti penzi letu kwa kuwa na mwingine wa pembeni na hata amempa mimba. Ajabu ni kuwa anasisitiza kuwa ananipenda na hataki kuniacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa dawa ya usaliti wa kimapenzi ni utengano. Hali kwamba mpenzi wako amempa mimba msichana mwingine ni thibitisho kuwa si mwaminifu kwako. Sikuelewi ukisema hataki kukuacha ilhali wewe ndiwe unayefaa kumuacha. Wangojea nini?

 

Nina umri wa miaka 16, nataka kuwa na mpenzi kama wenzangu shuleni

Nina umri wa miaka 16 na nitamaliza shule ya msingi mwaka huu. Wengi wa marafiki zangu wasichana wana wapenzi na mimi pia natamani kuwa na wangu. Je, nina haki ya kuwa na mpenzi kwa sasa?

Kupitia SMS

Katika umri wako huo haufai kuwa na mpenzi kwani wewe bado ni mtoto mdogo kiasi cha kuelewa maana hasa ya mapenzi. Pili unaema kuwa bado unasoma na ukianza kujihusisha na mapenzi utaharibu masomo. Subiri ukomae kisha umalize masomo yako ndipo ufikirie jambo hilo.

 

Nilianza urafiki na msichana lakini sasa ameanza kunihepa

Kuna msichana aliyekubali kuwa mpenzi wangu lakini baada ya siku chache akaanza kunihepa. Nampenda sana na sijui nitafanya nini ili kudumisha uhusiano wetu. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Kama ameamua kukuacha huwezi kumzuia kwa sababu yeye si mke wako na hata mke wako anaweza kuamua ametosha ndoa na kuondoka. Kubali uamuzi wake.

 

Mwanamume aliyeoa anataka kunioa ila nina mtoto mmoja

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 32 na nina mtoto mmoja ingawa sijaolewa. Nina uhusiano na mwanamume aliye na mke ambaye tunapendana sana na anataka kunioa mke wa pili. Waonaje?

Kupitia SMS

Ni kweli kuwa mapenzi yanaweza kumzuzua mtu hadi kupoteza macho na akili. Wewe bado ni mwanamke mchana na unaweza kupata mume wako mwenyewe badala ya kuolewa mke wa pili. Hata hivyo, wewe ni mtu mzima na una haki ya kuamua hatima ya maisha yako. Iwapo unahisi utatosheka kuwa mke wa pili na uweze kuishi maisha unayotaka, basi hakuna shida, kubali uolewe.