Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Alinitoroka nikiwa mjamzito sasa anataka turudiane

November 23rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu alinitoroka baada ya kunipa mimba. Nimepata mwingine anayenipenda na yuko tayari kunioa. Sasa wa awali amejua hayo na ameanza kunisumbua akitaka turudiane. Naomba ushauri wako tafadhali.

Kupitia SMS

Jamaa alitia doa uhusiano wenu kwa kukuacha wakati ambao ulimhitaji zaidi. Kwa sababu hiyo, huenda ikawa vigumu kwako kumuamini tena. Kwamba unahitaji ushauri wangu ni ishara kuwa bado uko na hisia kwake, na unashindwa iwapo itakuwa sawa kumrudia ama utaendelea na uhusiano wako mpya. Kama umetosheka na mapenzi ya uliye naye, huna sababu ya kumrudia mtu aliyekusaliti kwani anaweza kukuvunja moyo tena.

 

Naogopa kumfichulia hali yangu

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 21 ni nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miaka miwili. Anafanya kazi mji tofauti na hatujaonana kwa karibu miezi miwili. Sasa anataka nimtembelee lakini naongopa, kwa sababu nimeshindwa kumuelezea hali yangu ya kiafya. Naomba ushauri.

Kupitia SMS

Ingawa hujafafanua, ninaelewa kutokana na wasiwasi wako kwamba wewe ni mgonjwa, na umeshindwa kumfichulia mpenzi wako. Isitoshe, unahofia kuwa unaweza kumuambukiza kwa njia fulani. Ukweli ni kwamba uhusiano wenu hauwezi kuendelea bila nyinyi kuonana, labda iwe umeamua kujiondoa. Iwapo bado unataka kudumisha penzi lenu, itabidi umuambie mwenzako kila kitu ili mshauriane kuhusu hali hiyo.

 

Ghafla ameanza kutoa masharti

Niko katika uhusiano na mwanamke fulani. Tumekuwa tukishiriki mahaba bila kinga kwa sababu tunaaminiana. Sasa ameanza kushuku eti nina uhusiano wa pembeni, na anasisitiza tutumie kinga iwapo nataka tuendelee na uhusiano wetu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mapenzi yanahitaji uaminifu wa hali ya juu hasa wakati huu wa magonjwa hatari kama ukimwi. Kama mpenzi wako amekuamini kwa wakati ambao mmekuwa pamoja na sasa ameanza kukushuku, ni lazima ana sababu. Kwako kukubali ombi lake haina maana kwamba umekubali madai yake. Iwapo kweli huna uhusiano na mwanamke mwingine, mwambie hivyo. Lakini pia ukubali mtumie kinga kwa sasa hadi atakapothibitisha hilo, na kuweza kukuamini tena.

 

Tumekosa rada?

Shangazi, mimi ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi. Kuna kijana mwanafunzi wa kidato cha tatu anataka tuwe wapenzi. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Hakuna kati yenu anayeelewa maana ya mapenzi kwa sababu nyinyi bado ni watoto wadogo. Isitoshe, nyinyi ni wanafunzi, na mwaka ujao mnatarajiwa kuwa watahiniwa. Badala ya kupoteza wakati mkihangaisha mawazo yenu katika mambo ya mapenzi, mnafaa kuzingatia masomo. Mnahitaji kujiandaa ipasavyo kwa mitihani yenu mwakani. Wewe hasa uko mbali sana kimasomo na unafaa kusahau kabisa mambo ya mapenzi.

 

Hasira zikipanda ndo hivyo

Vipi shangazi? Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa mwaka mmoja sasa. Tatizo ni kwamba mwanamume mpenzi wangu amekuwa akinilalamikia eti niko na hasira nyingi. Sababu ni kwamba akinikosea mimi humfokea vikali, na ninaamini amekuwa akivumilia tu kwa sababu ananipenda kwa dhati.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo ni mwaminifu na anakupenda kwa dhati. Ameamua kukueleza anavyohisi kuhusu hasira zako, kwa sababu amejitolea kudumisha uhusiano kati yenu. Ni muhimu umsikie na utafute namna ya kudhibiti hasira zako kwake. La sivyo, anaweza kuchoshwa na tabia yako hiyo akaamua kukuacha. Kama wewe pia unampenda, jitahidi ujirekebishe.