Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Alionja asali akahepa, amerudi baada ya miaka miwili

March 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu wa kwanza maishani alionja asali kisha akaniacha. Miaka miwili baadaye amekuja kunibembeleza akitaka turudiane. Bado nampenda lakini simwamini. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni wazi kuwa unampenda kwa dhati mwanamume huyo na ndiyo maana unafikiria kumrudia licha ya aliyokutendea. Hata hivyo, nakutahadharisha kuwa kama alikutenda hayo wakati huo, anaweza kukutenda tena siku za usoni. Ni vyema ujue hivyo ukiamua kumpa tena moyo wako.

 

Kila mara anadai hana wakati

Kwako shangazi. Nina mpenzi tunayependana sana. Tatizo ni kuwa wakati ninapotamani kuwa naye hudai hana wakati. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi hujengwa na kudumishwa kupitia kila mmoja kumpenda mwenzake kama anavyojipenda. Ni vigumu kumpata mwenzako kila unapotaka kwani ana shughuli zingine maishani. Mnahitaji kupanga pamoja wakati wa kuonana.

 

Ni kigeugeu

Hujambo shangazi? Nina mpenzi lakini amekuwa kigeugeu. Kuna wakati nikimpigia simu anapuuza. Mara nyingi nimekuwa simpati kwa sababu ya kuzima simu. Ananipenda kweli ama ananichezea?

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi si hali ya kufa na kupona. Kama umeona dalili kwamba mwenzako hazingatii ipasavyo uhusiano wenu, una haki na uwezo wa kujiondoa na kutafuta uhusiano ambao unatimiza matarajio yako.

 

Ninahisi ananitumia vibaya kwa ulafi

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 22 na nimepata mchumba aliye tayari kunioa. Tatizo ni kuwa amekuwa akitaka mahaba kutoka kwangu kila wiki na ingawa ninampenda, ninahisi kwamba ninatumiwa vibaya. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Wachumba hufanya mambo kwa maelewano na kupitia hiari ya kila mmoja bila lazima. Una haki ya kuweka masharti yako kuhusu jinsi ya kuendesha uhusiano wenu. Mwambie mwenzako kuwa hufurahii mpango wake huo. Kama kweli anakupenda atakusikia ili kudumisha uhusiano wenu.

 

Amenidanganya

Shangazi ninahitaji ushauri wako. Kuna mwanamke tuliyejuana majuzi na tukapendana. Aliniambia alikuwa na mpenzi lakini waliachana. Hata hivyo nimechunguza na kugundua kuwa bado wako pamoja. Nifanyeje?

Sasa umejua kuwa mwanamke huyo alikuhadaa kwa hivyo ni juu yako kuamua iwapo utaendelea na uhusiano huo ama utajiondoa. Labda hata ana wanaume wengine na hujui.

 

Ninatamani kurudi

Shangazi nilikuwa na mpenzi niliyempenda sana lakini tulikosana mwaka uliopita. Tangu hapo aliacha kunipigia simu na nikimpigia anapuuza. Nimesikia ameonekana na mwingine lakini nampenda sana natamani turudiane. Nifanye nini?

Itakuwa vigumu kumpata tena mwanamume huyo kama kweli amepata mwingine. Hatua yake ya kuanzisha uhusiano mpya ni thibitisho kwamba amekata kauli kuwa uhusiano kati yenu umekwisha. Jaribu kutoa moyo wako kwake ili uweze kuendelea na maisha yako.

 

Simu hujibiwa na mwanamume

Kwako shangazi. Kuna mwanamke aliyekubali kuwa mpenzi wangu lakini kila nikimpigia simu inajibiwa na mwanamume. Nina wasiwasi, nishauri.

Kama hiyo ni simu yake, ina maana kuwa ana mpenzi mwingine na anafanya hivyo makusudi ili ujue kwa sababu hataki kukwambia mwenyewe. Usijidanganye kuwa una mpenzi.

 

Mume amepachika msichana mimba

Hujambo shangazi? Nimeolewa na nina mtoto mmoja. Nimegundua kuwa mume wangu amempachika mimba msichana fulani katika mtaa tunamoishi na hilo linaniuma sana. Nifanye nini ili kutuliza moyo wangu?

Hakuna ndoa isiyokuwa na changamoto zake. Ndoa hudumishwa kwa kuvumuliana na kusameheana. Inawezekana kwamba hiyo si tabia ya mume wako na kwamba aliteteleza tu. Jaribu kuzungumza naye uone kama anajuta na kuomba msamaha. Ikiwa hivyo msamehe. lakini pia akuhakikishie kuwa hatarudia.