Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Aliuteka moyo wangu sasa ameutema ghafla

July 3rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Kuna mrembo tuliyekutana katika hafla ya vijana miezi miwili iliyopita na tukapendana. Mapenzi yetu yalipamba moto kwa kipindi cha mwezi mmoja na kwa muda huo akaushika mateka moyo wangu. Licha ya yote hayo, ameniacha ghafla! Sasa nahuzinika kwa upweke na kukosa penzi lake. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, mapenzi kati yenu yalipamba moto kwa muda mfupi sana. Hilo si jambo la kawaida kwani hata hamkuwa mmefahamiana vyema. Hali hiyo mara nyingi hutokana na tamaa ingawa wahusika hudhani ni mapenzi. Inaonekana msichana huyo amegundua kuwa hana mapenzi ya dhati kwako na ndiyo maana ameamua kujiondoa mapema. Ushauri wangu ni kuwa ukubali kuwa si wako tena ndipo uweze kufungua moyo wako kwa mwingine.

 

Nimempa mimba na sitaki kuoa sasa

Shangazi nahitaji ushauri wako. Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye ninampenda sana. Hata hivyo, nimempa mimba bahati mbaya na siko tayari kumuoa kwa sasa. Hofu yangu ni kuwa wazazi wake wakijua watazua balaa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Nimetumia nafasi na wakati mwingi katika safu hii kutahadharisha wapenzi dhidi ya kupata watoto kabla ya ndoa. Badala yake, nimekuwa nikiwashauri wasioweza kuvumilia watumie kinga ili kuepuka mimba na magonjwa ya zinaa. Licha ya juhudi zangu hizo, bado watu wanaendelea kuja kwangu wakitaka ushauri kuhusu mimba zilizopatikana ‘kwa bahati mbaya’. Umempa mimba binti ya wenyewe. Huo ni mzigo wako na ni lazima uwajibike. Kama hutaki balaa, nenda kwa wazazi wa mpenzi wako ujitambulishe kisha uwahakikishie kuwa utamuoa binti yao kabla au baada ya kujifungua.

 

Nina hofu ‘mafisi’ watanipokonya mke

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 26 na nilioa hivi majuzi. Hata hivyo, kuna jambo ambalo linanikera sana moyoni kuhusu ndoa yangu. Mke wangu ni mrembo sana na kila anakopitia wanaume humfuata kama nyuki wakimtongoza. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huwezi kumlaumu mke wako kwa sababu ya urembo wake. Maumbile ni ya Mungu na ninaamini wewe pia ulimpenda kwa sababu ni mrembo. Unachofaa kujua ni kwamba hilo si tatizo lako pekee bali la wanaume wote walio na wake warembo. Mwanamke mrembo ni lazima atatongozwa awe na mume au la. Lakini hilo halifai kuwa tatizo, bora tu unamwamini mke wako naye athamini na kuheshimu ndoa yenu. Wanaomtaka watamfuata hadi wachoke.

 

Nimethibitisha anaye wa pembeni

Kwako shangazi. Kuna msichana tunayependana lakini nimegundua ana mwanamume mwingine wa pembeni. Tumegombana mara kadha kuhusu jumbe za kimapenzi kutoka kwa mwanamume huyo huku akidai hakuna kinachoendelea kati yao lakini sasa nimethibitisha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huna la kufanya isipokuwa tu kuachana na msichana huyo kwani unasema umethibitisha kuwa ana mpenzi mwingine. Ninahisi kuwa anampenda huyo mwingine zaidi yako la sivyo angeachana naye ulipogundua mpango huo. Badala yake, aliamua kukuhadaa kuwa hakuna kinachoendelea kati yao. Usipoteze wakati zaidi kwake.

 

Shangazi nisaidie kupata kiosha roho

Habari yako shangazi? Jina langu ni Frederick na ninatafuta mwanamke wa kuoa. Nina umri wa miaka 26. Nisaidie tafadhali.

Kupitia SMS

Shughuli ya kutafuta mpenzi ni suala la kibinafsi hivyo haihitaji msaada kutoka kwa yeyote yule. Ni wajibu wako kumtafuta anayevutia hisia zako kimapenzi kisha kumdokezea unavyohisi. Mkipatana, hewala, utakuwa umetimiza nia yako. Kazi kwako kaka Frederick.