SHANGAZI AKUJIBU: Alivunja uhusiano wetu baada ya asali, naumia!

SHANGAZI AKUJIBU: Alivunja uhusiano wetu baada ya asali, naumia!

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Nilikuwa nimemwambia kuwa sitamuonjesha asali hadi siku ambayo nitakuwa mke wake. Hata hivyo, amekuwa akinisukuma na kufikia hivi majuzi msimamo wangu mkali ulitishia kuvunja uhusiano wetu hadi nikasalimu amri. Siku moja baadaye mpenzi wangu alinitumia SMS akisema ameamua kuvunja uhusiano wetu. Nampenda sana na uamuzi wake huo unanikosesha usingizi hasa baada ya kukubali ombi lake. Tafadhali naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa mwanamume huyo hakuwa na haja na uhusiano bali alitaka tu kulamba asali na baada ya kuipata ameamua kutoweka. Ushauri wangu umekuwa kwamba mapenzi yanafaa tu katika ndoa na walio na mapenzi ya dhati huvumilia. Ninaamini umejifunza kutoka kwake na wakati mwingine utakuwa mwangalifu.

 

Mpenzi ameamua kurudi kwa mke wake

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 32 na bado sijaolewa. Mpenzi wangu ni mwanamume ambaye alikuwa ameoa lakini akaachana na mke wake. Alikuwa ameniahidi kwamba tutaoana mwaka huu lakini mambo yamebadilika ghafla. Kisa ni kwamba mpenzi wangu ameamua kurudiana na mke wake. Hatua yake hiyo imeniacha hali mbaya kwani tayari nilikuwa nimemjulisha kwa jamaa na marafiki zangu na sijui watasema nini. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Hatua ya ghafla ambayo mpenzi wako amechukua ni ishara kwamba anampenda mke wake na hakua amemtoa moyoni hata baada ya wao kuachana. Huenda hata alitumia uhusiano wenu kumtia wivu mke wake ili akubali warudiane. Ukweli ni kuwa huwezi kubadili uamuzi wake huo. Usijali kuhusu watakayosema jamaa na marafiki kwa sababu hiyo ni hali ya kawaida katika mahusiano.

 

Anahofia wazazi wake hawatanikubali

Habari zako shangazi? Nina umri wa miaka 46 na bado sijaolewa ingawa nina watoto wawili. Nina uhusiano wa kimapenzi na mwanamume wa miaka 29 na ninaamini anaweza kuwa mume mzuri kwangu licha ya umri wake mdogo. Nimezungumza naye kuhusu jambo hilo na amekubali ingawa shingo upande kwa sababu anahofia kwamba wazazi wake watapinga mpango huo. Anasema pia marafiki zake watamsema. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa umri si hoja katika mapenzi na ndoa, nahisi kuna upungufu fulani katika uhusiano wenu ambao unaweza kuathiri vibaya mpango huo. Wewe ndiye umependekeza kuhusu mpango wa ndoa. Inawezekana kwamba hakuwa na mpango huo na ndiyo maana amekubali shingo upande. Jambo lingine la kuonyesha kuwa hataki ndoa ni kuwaingiza wazazi na marafiki zake katika uhusiano wenu. Tafadhali usimlazimishe.

 

Hili jimama katika ndoa limeniganda kama kupe

Kwako shangazi. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 26. Nina mpenzi na sijawahi kufikiria kumsaliti kimapenzi. Kuna mwanamke jirani yangu mtaani ambaye ananiandama akidai ananipenda na anataka tuwe wapenzi. Ajabu ni kwamba ameolewa na anajua vizuri kuwa nina mpenzi kwa sababu amemuona akinitembelea nyumbani kwangu. Nimemwambia siwezi lakini hasikii. Juzi alikuja kwangu usiku akiomba tuzungumze nikakataa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Tabia ya mwanamke huyo inaonyesha kwamba ndoa yake ina matatizo na anatafuta mtu wa kumliwaza tu. Madai yake kwamba anakupenda ni ya uongo kwa sababu ana mume na anajua wewe pia una mpenzi. Usikubali kutumiwa kwa njia hiyo. Itabidi pia umwambie akome kuja kwako kwa sababu mume wake ama mpenzi wako akimpata huko atafikiria mna uhusiano. Muonye pia kwamba asipoacha kukufuata utamwambia mume wake.

You can share this post!

MAZINGIRA NA SAYANSI: Moshi wa mafuta ya dizeli...

Nyani wahangaisha wakazi majumbani

adminleo