Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Aliyeniahidi tutaoana amenyakuliwa na tajiri

March 14th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi tangu tulipoingia chuo kikuu hadi tukamaliza ameniacha kwa mataa. Nimeshangaa kugundua kuwa ameshikana na mwanamume tajiri ambaye ana familia. Nilipomuuliza aliniambia wazi kuwa hawezi kuendeleza uhusiano na mtu ambaye hana kazi wala hajui atakapoipata. Nilidhani atakuwa mwenzangu maishani na hatua yake hiyo imeumiza sana hisia zangu. Naomba ushauri wako tafadhali.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi si wa kudumu na ndiyo sababu unafaa kuwa tayari kwa uamuzi wowote ule, wakati wowote ule kutoka kwa mwenzako. Ukweli ni kwamba mwanamke huyo ametema penzi lako kwa ajili ya pesa. Ingawa unaumia moyoni kwa kumpoteza, itabidi ukubali na uangalie mbele kwani huo si mwisho wa maisha.

 

Amekataa kabisa kunisamehe

Hujambo shangazi? Nilikosana majuzi na mpenzi wangu kuhusu jambo fulani na tukaachana. Hata hivyo tumekuwa tukiwasilina kwa simu na nimemuomba msamaha nikitaka turudiane amekataa. Sijui nitafanya nini kwani ninampenda sana.

Kupitia SMS

Hali kwamba hajakatiza mawasiliano ni dalili nzuri. Jaribu kumpa muda atulize hasira uone kama atakusamehe. Lakini pia kuwa tayari kwa chochote kile kwa sababu inawezekana kuwa ameamua hataki kurudi katika uhusiano huo na labda amepata mwingine.

 

Mke wa wenyewe anataka nimzalie

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 26 na nimeokoka. Bado sijaoa na ninaendelea kutafuta mke. Kuna mwanamke ambaye tunahudhuria kanisa moja ambaye amekuwa akinitaka. Ameolewa lakini ananiambia kuwa mumewe hana uwezo kumzalisha na anataka nimzalie mtoto. Je, nitakosea kumsaidia?

Kupitia SMS

Kama kweli wewe umeokoka, bila shaka unajua kuwa ni dhambi kumtimizia mwanamke huyo ombi lake. Dini inakukukataza, sio tu kuwa na uhusiano na wake wa wenyewe, bali pia kushiriki mapenzi kabla ya ndoa. Kama unaheshimu dini na Mungu wako, basi jiepushe na jambo hilo.

 

Hanipi pesa hadi nimuombe

Vipi shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa lakini nahisi kwamba hanifai. Sababu ni kuwa hawezi kunipatia pesa za mahitaji yangu kwa hiari yake ni lazima nimuombe. Nimejaribu kumrekebisha lakini nimeshindwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Inawezekana kuwa mwanamume huyo hajui jinsi ya kujenga na kutunza uhusiano ama ni mtu mchoyo tu. Uhusiano ni chaguo la mtu binafsi kwa hivyo kama unahisi huyo siye mtu ambaye ungependa kuishi naye unaweza kujiondoa katika uhusiano huo.

 

Nashindwa kueleza mapenzi yangu kwa aliyenizuzua

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 24. Kuna mwanamke fulani ambaye amenifanya nikose usingizi usiku nikimfikiria kwa sababu nampenda sana ingawa hajui. Nimekuwa nikipanga kumwambia lakini kila tukikutana maneno hupotea. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Wewe ndiye umempenda mrembo huyo na ni wewe tu utakayemwelezea hisia zako. Usipofanya hivyo uhusiano wenu utabakia ndoto tu. Weka woga kando, kisha umuite faraghani umwelezee uliyo nayo moyoni.

 

Yeye hunitafuta tu wakati anataka kuhudumiwa

Shangazi nafikiri nia ya mwanamume mpenzi wangu ni kunitumia tu na hana nia njema kwangu. Sababu ni kuwa tumejuana kwa muda mfupi tu na huwa ananipigia simu tu akitaka nimhudumie. Tukimaliza hilo yeye hutoweka na kunyamaza hadi wakati mwingine anaponihitaji. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Nitakulaumu wewe kwa kukubali kutumiwa na mtu ambaye mmejuana kwa muda mfupi tu. Hata kama unampenda namna gani, unafaa kujuzuia na kujipa wakati wa kutosha kumfahamu vyema na kujua nia yake kwako. Ushauri wangu ni kuwa ukatize huduma hizo unazompa kama njia ya kujua iwapo anakupenda kwa dhati.