Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Aliyenioa hanipendi, sijui nihamie kwa mpenzi wa kale?

August 6th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nimeolewa kwa miaka miwili na niliamua kuwa sitapata mtoto kwanza kwani nimekuwa na shaka kuhusu iwapo mume wangu ananipenda kwa dhati. Katika muda ambao tumekuwa pamoja nimethibitisha kuwa hanipendi. Kuna mwanamume aliyekuwa akinitaka hata kabla sijaolewa na bado ananipenda kwani hajaoa. Je, nitakosea kumuacha niliye naye niolewe tena?

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini ulikubali kuolewa na mwanamume huyo ilhali hukuwa na hakika kuhusu mapenzi yake kwako. Hata hivyo, ni bahati kwamba umetambua kosa lako mapema na itakuwa vyema ufuate moyo wako. Ni haki yako kujitafutia maisha yanayoridhisha moyo wako kwa hivyo hutakosea kumuacha mume wako ili kutafuta kwa mwingine. Keti naye chini umwelezee mpango wako huo.

 

Ningali shule ila nimezalisha mke wa wenyewe, nifanyeje?

Shikamoo shangazi! Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 20 na bado ninasoma. Nimekuwa na uhusiano na mke wa mwenyewe kwa miaka mitatu sasa na tumezaa mtoto pamoja. Wazazi wangu wamejua kuhusu uhusiano huo na wanapinga vikali. Juzi walienda kwake wakamtukana sana na sasa amekasirika anatishia kuniacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Naona unacheza na maisha yako mtoto wewe. Kwa umri wako huo unawezaje kuanzisha uhusiano na mke wa mwenyewe na kuzaa pamoja? Isitoshe, bado wewe ni mwanafunzi na huna hunani unawategemea wazazi wako. Ningekuwa wao ningekuchara viboko mpaka upate adabu. Kama umeonywa na wazazi wako na hujasikia, nami nakuonya tena. Mkome mke wa mwenyewe. Siku mumewe akijua utakuwa kwenye balaa kubwa.

 

Tabia yake yaniudhi sana, sasa apakua chungu cha jirani!

Shangazi nimeolewa lakini mume wangu ananiudhi kwa tabia yake ya kuwa na ‘mipango ya kando’. Hivi sasa ameshikana na mwanamke jirani yetu mtaani na ninaona aibu sana kwani majirani wengi wamejua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni aibu kubwa sio kwako tu bali pia kwake kwani majirani wanaojua tabia zake hawawezi kumheshimu. Nimesema mara nyingi hapakwamba ndoa ikifikia hapo ni heri mtu kujiondoa.

 

Nataka kuacha kazi nimkaribie mpenzi

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi tunayependana sana. Kila mmoja wetu anafanya kazi mbali na mwenzake na imekuwa changamoto kubwa kwetu kuonana. Wakati mwingine huwa nafikiria kuacha kazi ili nikaishi karibu naye. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi unahitaji wahusika kuonana kila siku ikiwezekana. Lakini mara nyingi hilo haliwezekani kutokana na changamoto nyingi za maisha, ikiwemo kazi na inabidi wahusika wavumilie bora tu wadumishe uhusiano wao. Kamwe, usiache kazi kufuata mapenzi.

 

Naogopa wazazi watamkataa

Hujambo shangazi? Nina uhusiano na mwanamume ambaye ninampenda kwa moyo wangu wote. Bado sijawaambia wazazi wangu kwa hofu kwamba wakijua anatoka jamii tofauti na yangu watamkataa. Nishauri.

Kupitia SMS

Ukishikilia kuwa utachagua mpenzi au mume kupitia idhini ya wazazi au jamaa zako utakosea sana. Huu si wakati wa watu kuzingatia makabila yao wanapoamua kuaoana. Waambie wazi wazazi wako kuwa umempenda mwanaume huyo bila kujali kabila lake na huna mpango wa kutafuta mwingine.

 

Nimependana na mume wa wenyewe na penzi limenoga, utanishauri vipi?

Shangazi nimechanganyikiwa. Nina uhusiano na mume wa mtu ambaye tunapendana sana. Nina umri wa miaka 22 naye ana umri wa miaka 38. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba umeamua kushikana na mume wa mwenyewe badala ya kutafuta wako kwani wewe ni mwanamke mchanga. Mwanamume huyo anakuhadaa eti anakupenda lakini atakutumia na hatimaye akuache atulie kwa mke wake. Shauri yako.