Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ameanza masharti ilhali penzi bado changa

November 9th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI sielewi iwapo mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miezi miwili pekee, ameingiwa na wazimu ama ni nini. Anataka niwe nikimtembelea kila siku, nikikosa ananitishia maisha. Juzi nilikosa kumtembelea, akaja kwangu usiku amebeba panga anataka kunishambulia, lakini nikatoroka. Kisa hicho kimenishtua sana na simtaki tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Hayo yake si mapenzi bali ni wazimu. Ni ajabu kwamba amekuwekea lazima ya kumtembelea ilhali kwa kawaida ndiye anayefaa kukutembelea. Hatua yake ya kukuvamia nyumbani kwako kwa panga pia inatia hofu. Huyo anaweza kukudhuru, muhimu umuepuke haraka iwezekanavyo. Kama anajua unakoishi itabidi uhame na pia ubadilishe nambari yako ya simu.

 

Sijui kwa nini mpenzi wangu haniamini tena. Analalamika eti natoka na kijana mwingine na hiyo si kweli

Hujambo shangazi? Kuna kijana mpenzi wangu lakini haniamini. Amekuwa akinilaumu eti ninamcheza na kijana mwingine, wala hamna ukweli wowote hapo. Nisipomtembelea pia huwa anakasirika. Nifanye nini?

JANET, Kupitia SMS

Hakuna haja ya kuwa katika uhusiano usiokuwa na uaminifu, hasa kama mwenzako anakushuku bila sababu. Huyo mpenzi wako anasumbuliwa na wivu, na asipobadilika aanze kukuamini basi mtaendelea kusumbuana tu. Mwambie kama hakuamini muachane kila mtu atafute mwingine.

 

Barafu wa moyo wangu hana shughuli na mimi siku hizi kiasi kwamba hata kunipigia simu imekuwa balaa

Nimekuwa na mpenzi kwa miezi mitano na ninampenda sana lakini ghafla naona amebadilika ni kama hana shughuli na mimi tena. Kinyume na awali, siku hizi ni mimi ninayemtafuta kwa simu ili kumjulia hali. Hii sasa ni wiki ya tatu hatujaonana. Shangazi, je, ananipenda kweli?

Kupitia SMS

Tabia ya mpenzi wako si ya kawaida hususan katika uhusiano mchanga kama wenu. Huenda kwa muda huo mfupi ambao mmekuwa pamoja amegundua kuwa hana mapenzi ya dhati kwako, na ameamua kujiondoa katika uhusiano lakini anashindwa kukwambia. Mtafute umuulize ili ujue msimamo wake.

 

Nuksi ya kukosana na wanawake imeniandamana tangu tuachane na mama watoto

Mambo shangazi? Nilikuwa nimeoa lakini nilikosana na mke wangu. Tuliachana miaka mitatu iliyopita. Tangu wakati huo nimekuwa nikitafuta mke lakini kila ninayepata tunakwaruzana. Kufikia sasa, nimekutana na wanawake kumi ambao tumekosana baada ya kuwa pamoja kwa muda mfupi tu. Nifanyeje ili nidumu na mwanamke katika uhusiano?

Kupitia SMS

Hali yako ya kukosana na kila mwanamke mnayekutana naye inatia shaka. Ni ajabu kwamba umekutana na wanawake hao wote, na hakuna hata mmoja amekufaa kama mke ili uweze kutulia. Labda kuna udhaifu fulani katika nafsi yako ambayo inawafanya wanawake wakutoroke. Chunguza ujue ni wapi ilipo shida ili ujirekebishe. Unaweza pia kuwauliza baadhi ya wanawake mliokosana, wakueleze nini kiliwafukuza.

 

Mpenzi anataka nimjulishe kwa wazazi. Tatizo ni kuwa, sina wazazi, na anayenilea atapinga uhusiano wetu

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 19 na huu ndiyo mwaka wangu wa mwisho katika shule ya upili. Mpenzi wangu ana umri wa miaka 24, na tumekuwa pamoja kwa karibu mwaka mmoja. Amenitambulisha kwa mamake lakini bado sijampeleka kwetu. Mama yangu aliaga dunia nikiwa mchanga na nimelelewa na nyanya. Mpenzi anataka nimtambulishe kwa nyanya lakini nahofia atapinga uhusiano wetu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Iwapo nyanya atapinga uhusiano wenu, atafanya hivyo kwa sababu mbili. Kwanza, wewe bado ni mwanafunzi. Hata kama unamaliza shule ya upili, unahitaji masomo ya ziada ndipo uweze kujitegemea na kumtunza nyanyako jinsi ambavyo amekutunza tangu utotoni. Pili, umri wako bado mdogo, ni mapema sana kwako kuingilia mapenzi. Zungumza na mpenzi wako akupe muda wa kujiimarisha kimasomo na pia kukomaa kimwili na kiakili.