Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Amekubali kuwa wangu, sharti ni nimpe pesa!

April 24th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Kuna mwanamke ninayemtaka na amenizungusha kwa muda sasa. Hatimaye alinipigia simu juzi akaniomba tukutane maskani fulani ya starehe. Baada kubugia vinywaji kadhaa, aliniambia atakubali tuwe wapenzi bora tu niwe nikimpa kiwango fulani cha pesa kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya mahitaji yake. Je, hayo kweli ni mapenzi?

Kupitia SMS

Ninaamini unahitaji mpenzi aliye na mapenzi ya dhati kwako. Kama ndivyo, huyo siye kwani tayari amekuonyesha wazi kuwa pesa ndizo muhimu zaidi kwake.

Miaka saba sasa ndiyo asema kijiko kidogo?

Hujambo shangazi? Nimeoa na mimi na mke wangu tumeishi kwa miaka saba. Nashangaa kwamba mke wangu ameanza kulalamika eti kijiko changu ni kidogo hakimlishi akashiba. Lalama zake hizo zinanifanya nishuku kwamba ameanza kupakuliwa nje. Waonaje wewe?

Kupitia SMS

Una sababu ya kutatizika kuhusu kauli ya mke wako hasa kwa sababu mmeishi pamoja kwa miaka hiyo yote na hajawahi kulalamika tena kuhusu hali hiyo. Hata hivyo, siwezi kusema kwa hakika kuwa ameanza kwenda nje. Ushauri wangu ni kwamba ujipe muda uchunguze mienendo ila yake ili ujue kinachoendelea.

 

Nimegundua huonana kisiri na dume jirani

Hujambo shangazi? Nilioa mwaka jana lakini nilitengana na mke wangu majuzi nilipogundua amekuwa akiwasiliana na hata kukutana kisiri na mwanaume jirani yetu. Nimeamua kuwa simtaki tena lakini kwanza naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hali kwamba mke wako amekuwa akiwasiliana na kukutana kisiri na jirani yenu inatia shaka kwani ni dalili za kutokuwa mwaminifu kwako. Kama unaamini mkirudiana hamuwezi kuishi vizuri itakuwa heri zaidi muachane.

 

Mrembo ameniambia anapenda hela zangu

Vipi shangazi? Kuna jambo ambalo msichana mpenzi wangu ameniambia nikashangaa. Eti ananipenda tu kwa sababu nina pesa na kwamba nitakapokuwa sina ataniacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Hiyo ina maana kuwa msichana huyo hakupendi bali anapenda pesa zako tu na inaonekana kwamba hiyo kwako si hoja. Ushauri wangu ni kuwa uzingatie kauli yake ili utakapoishiwa usianze kulia akikutema.

Wazazi hawataki kusikia nina mpenzi

Mambo shangazi. Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nina uhusiano na msichana aliyemaliza masomo mwaka jana. Wazazi wangu wamejua na wamenionya vikali kwamba nivunje uhusiano huo. Nampenda sana msichana huyo na sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Sababu hasa ya wazazi wako kupinga uhusiano huo ni kuwa wewe bado ni mwanafunzi na ukiendelea nao utaathiri vibaya masomo yako. Kumbuka kuwa mpenzi wako amemaliza masomo na hana chochote cha kupoteza. Nakushauri utii ushauri wa wazazi wako iwapo unataka maisha mema.

Nahisi ananitaka

Kwako shangazi. Kuna mwanamke ambaye amenasa moyo wangu na inaonekana yeye pia ana hisia kwangu kwani tunapokutana hunichangamkia sana utadhani tumejuana kwa muda mrefu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako ni wazi kuwa umeona dalili za mwanamke huyo kuvutiwa kwako kimahaba. Hatua unayofaa kuchukua sasa ni kumdokezea hisia zako ili naye apate nafasi ya kuungama iwapo anahisi vivyo hivyo.

Hanipi burudani huyu

Kwako shangazi. Nina mpenzi ninayempenda kwa dhati lakini kila nikitaka burudani hukataa kwa kunipa sababu nyingi ambazo hazina maana.

Kupitia SMS

Unalalamika kama kwamba hiyo burudani ni haki yako. Huyo ni mpenzi wako tu, si mke wako na ana haki ya kukupa na pia kukunyima hiyo burudani. Kama kweli unampenda, nenda taratibu kuhusiana na suala hilo la sivyo utampoteza.