Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ameniacha sababu simudu mahitaji yake mengi

June 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Pongezi kwa kazi nzuri unayofanya katika ukumbi huu. Nimekuja kwako kuomba ushauri wako. Mwanamke mpenzi wangu ninayempenda kwa moyo wangu wote ameniacha kwa sababu nimeshindwa kutimiza mahitaji yake mengi ya kifedha. Mapato yangu ni duni na nimejaribu kadiri ya uwezo wangu kumtimizia ninayoweza. Lakini mahitaji yake yanaongezeka kila siku. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sidhani mwanamke huyo ana mapenzi ya dhati kwako ingawa anadai anakupenda. Sababu ni kwamba mapenzi ya dhati hayana ubinafsi. Inaonekana kuwa anajali zaidi nafsi yake na ndiyo maana ameweka mahitaji yake mbele. Hiyo ina maana kuwa uhusiano wenu utategemea uwezo wako wa kukidhi mahitaji yake na utakaposhindwa huo utakuwa mwisho wake.

 

Baba zetu marafiki wa dhati, ni kosa tukiwa wapenzi?

Hujambo shangazi? Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu na nina umri wa miaka 22. Nina mpenzi ninayempenda sana lakini nimegundua kuwa baba yake na baba yangu ni marafiki wakubwa. Je, kuna makosa tukiwa wapenzi?

Kupitia SMS

Urafiki wa wazazi wenu hauwezi kuathiri kwa vyovyote uhusiano wenu wa kimapenzi. Badala yake, urafiki wao unafaa kuchochea zaidi uhusiano wenu kwa sababu wakati ukifika kwenu kufunga ndoa haitakuwa vigumu kwa kila mmoja wenu kumtambulisha mwenzake kwa baba yake kwa sababu tayari wanajuana.

 

Je, kuna njia ya mkato kupata jiko?

Mimi ni mwanaume mwenye umri wa miaka 32. Ninataka sana kuoa lakini nina shida moja. Imekuwa vigumu kwangu kuvutiwa na wanawake wengi ninaokutana nao kwani hawatoshelezi maumbile na tabia za mke ambaye ninataka. Nahisi itanichukua muda kutafuta ilhali nahisi umri umezidi na ninataka kuoa ili nitulie. Je, kuna njia ya mkato?

Kupitia SMS

Kwanza, kakuna kitu kizuri kinachopatikana kwa urahisi. Kwa hivyo, ni lazima ujitolee na uwe na subira unapotafuta mke mwenye sifa unazotaka. Pili, ukiendelea kutafuta, ningependa kukuonya kuwa itakuwa vigumu kumpata mwenye sifa zote unazotaka kwani hakuna mtu mkamilifu. Kila la heri.

 

Anisukuma tuwe wapenzi na sitaki

Shangazi ni matumaini yangu kwamba wewe ni mzima. Tafadhali naomba unisaidie. Kuna msichana anayenitaka lakini ana marafiki chungu nzima wa kiume. Amekuwa akinisukuma tuwe wapenzi lakini mimi simtaki. Nishauri.

Kupitia SMS

Si hatia kwa mwanamke kuwa na marafiki wa kiume kwani hiyo haina maana kuwa ni wapenzi wake. Kama yeye mwenyewe ndiye anayekusukuma, hiyo ina maana kuwa hana mpenzi, wanaume unaomuona nao ni marafiki tu. Hiyo isiwe sababu yako ya kumkataa, labda useme huna hisia kwake.

 

Washinikiza harusi lakini siko tayari sababu sina mahari

Vipi shangazi? Nina mwanamke tunayependana na nimeamua ndiye atakuwa mke wangu. Watu wa familia yake wanajua kuhusu uhusiano wetu na wanatuhimiza tufunge ndoa kwa sababu tumechumbiana kwa muda mrefu. Tatizo ni kwamba siko tayari kwa sasa kwani ni lazima watahitaji mahari. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ndoa inahitaji mpango. Ni kweli huwezi kumuoa mpenzi wako bila kumlipia hata kama ni sehemu ya mahari. Ninaamini kuwa mchumba wako anaelewa hali yako kwa hivyo shauriana naye ili awaombe wazazi wake wawe na subira hadi mtakapokuwa tayari.

 

Nahisi nina mkosi, wapenzi nipatao hawadumu kamwe

Shangazi nahisi kama kwamba nina mkosi katika mahusiano ya kimapenzi. Sababu ni kuwa nimekuwa nikipata wapenzi kwa urahisi lakini wananiacha baada ya muda mfupi tu. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi hudumu kutokana na kutosheka kwa wahusika. Wapenzi wanaokuacha huwa na sababu za kufanya hivyo wala si mkosi. Labda utakutana na wengine wakuache na hiyo ni hali ya kawaida kwa wanaotafuta wachumba. Hatimaye utampata wako muishi pamoja.