Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Amenigandia, hali halali eti atanifia kimahaba!

April 16th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Ananipenda sana na ameniambia mara kadhaa kuwa hatawahi kuniacha maisha yake yote. Mimi sina hakika kuhusu maisha yetu baadaye lakini inaonekana yeye amekata kauli. Sababu ni kuwa tumekosana na kuachana mara kadhaa na bado ananirudia. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati hatimaye hufikia kiwango cha ndoa. Ni jambo kushangaza kwamba umekuwa ukimhadaa mpenzi wako kuwa unampenda ilhali huna nia ya kufunga ndoa naye. Matamshi yake ni thibitisho kuwa amekupa moyo wake wote na kama huna mpango wa kuishi naye ni heri umwambie sasa.

 

Shangazi naomba kibarua nifae familia

Hujambo shangazi? Tafadhali nina ombi kwako na ninatumai kuwa utanifaa. Nina mke na watoto na nina shida kubwa ya kuwakimu baada ya kuachishwa kazi hivi majuzi. Je, unaweza kunitafutia kazi yoyote ile hata kama ni ya kibarua?

Kupitia SMS

Samahani, ukumbi huu hasa ni wa kutoa ushauri wala si wa kutafutia watu kazi. Hata hivyo, kwa sasa sina mahali ninapoweza kukuelekeza. Usife moyo, endelea kutafuta, hatimaye utapata.

Amenipachika mimba akanitema, naumia moyoni!

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 16 na ninasoma katika shule ya upili na kuna kijana tunayependana. Juzi nilimtembelea nyumbani kwake na akanishawishi nimburudishe. Nimegundua nina mimba yake na sasa hataki hata kunioa. Nisaidie.

Kupitia SMS

Nimeonya mara nyingi katika ukumbi huu na ninaamini kuwa wewe pia umeonywa na wazazi wako kuwa katika umri wako hufai kujihusisha na mahaba. Pili, wewe ni mwanafunzi na unafaa kuzingatia masomo yako badala kuzurura huku na kule ukitafuta mapenzi. Ulitoka kwenu mwenyewe kiguu na njia hadi nyumbani kwa kijana huyo na ukapata ulichotaka. Beba mzigo wako.

 

Mpenzi anashinda mno na rafiki yangu

Shikamoo shangazi! Kuna kijana jirani yetu mtaani anayedai ananipenda lakini nimemuona mara kadhaa akitembea na msichana rafiki yangu na ninashuku kuwa wana uhusiano. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni muhimu kuingia katika uhusiano ukiwa na hakika kuwa ni kati yenu wawili tu na hakuna mtu wa tatu. Ushauri wangu ni kuwa uchunguze kwanza ujue kinachoendelea kati yao ndipo ujue iwapo utakubali au utakataa ombi lake.

Nahisi nimepevuka, naotea demu mmoja kazini

Za kwako shangazi? Nina umri wa miaka 24 na bado sijapata mpenzi. Kuna mwanamke tunayefanya kazi pamoja na tumekuwa marafiki kwa miezi kadhaa sasa. Nimeanza kuvutiwa pia lakini sina hakika. Nishauri.

Kupitia SMS

Si jambo la kawaida kwa wanawake kutangaza hisia zao za kimapenzi kwa wanaume. Kama kweli anakupenda na una hakika kuhusu hilo, ni lazima amekuonyesha dalili akitarajia kwamba utachukua hatua. Wewe nawe unasema huna hakika kuhusu hisia zako kwake. Shikilia urafiki huo tu hadi utakapokuwa na hakika kuwa ndiye chaguo la moyo wako ndipo utakapomwambia.

Amenioa majuzi ila nimebaini kuwa waliachana na mwingine, nina hofu!

Hujambo shangazi? Niliolewa majuzi na nimepata habari kuwa mume wangu alikuwa ameoa na wakaachana na mkewe. Hajaniambia alikuwa ameoa ingawa sijamuuliza na nina wasiwasi kwani sijui waliachana kwa nini na kwa masharti gani. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni muhimu kumjua vizuri mchumba wako, sio jina tu wala kwao, bali pia maisha yake ya awali. Ulifaa kuchunguza mapema kujua iwapo mwanamume huyo amewahi kuwa na mke. Ni muhimu umuulize sasa ili akuhakikishie kuwa ameachana kabisa na mkewe wa awali asije akaingilia maisha yenu.