Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Amesaliti penzi na hata kapata ujauzito, nishauri

March 27th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa miaka minne sasa na amekuwa akifanya kazi sehemu mbalimbali. Ilifika wakati ikawa nikimpigia simu ama kumtumia SMS wakati wa usiku hajibu hadi asubuhi. Juzi alinipigia simu kuungama kwamba amesaliti penzi letu na alitaka kuniomba msamaha. Aliniambia ana mimba ya mwanamume mwingine na hataki kuolewa naye kwa sababu mimi ndiye chaguo lake maishani. Nampenda na nimeamua kumsamehe lakini siko tayari kumuoa kwa sasa kwa sababu sina kazi nzuri wala sitaki atoe mimba hiyo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni vyema kwamba mpenzi wako ameungama makosa yake nawe umeamua kumsamehe. Kama mwenzako anafanya kazi, mnaweza kukubaliana ajifungue kwanza kisha msaidiane kumlea mtoto hadi utakapokuwa tayari kumuoa. Maisha ya siku hizi ni kusaidiana na hasa ni rahisi kwa watu wanaopendana. Keti chini naye mshauriane kuhusu suala hilo na bila shaka mtapata mwelekeo.

 

Tulikosana ila moyo umekwama kwake

Hujambo shangazi. Nina umri wa miaka 22 na kuna msichana tuliyependana sana lakini tukakosana. Bado ninampenda kwa moyo wangu wote na nimeshindwa kabisa kutafuta mwingine. Tafadhali nipe ushauri.

Kupitia SMS

Hujaelezea kilichowafanya mkosane wala aliyekosea mwenzake. Kama ndiye aliyekukosea, mtafute umsamehe ili mrudiane. Kama wewe ndiye uliyemkosea, vile vile mtafute umuombe msamaha uone kama atakubali mrudiane. Akikataa, itabidi ukubali uamuzi wake na hatimaye utamsahau na kuweza kuendelea na maisha yako.

 

Nimechoshwa na karata anayocheza

Habari zako shangazi? Nilioa mwanamke bila kujua kuwa alikuwa ameolewa na mwanamume mwingine na walipotengana alimuachia mumewe watoto wao wanne. Nilipogundua, tuligombana na akarudi kwa mumewe. Mwaka mmoja baadaye, anataka kurudi kwangu ilhali akiondoka alikuwa amesisitiza kuwa hatawahi kurudi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Nahisi kuwa mwanamke huyo amechanganyikiwa, hajui anachotaka maishani na kumpa nafasi tena katika maisha yako ni kujitafutia balaa tu. Tabia yake hiyo inaonyesha ndoa yake imekuwa na matatizo na sasa anataka kukutumia kama mahali pa kukimbilia kila anapokosa amani katika ndoa yake. Muepuke kabisa.

 

Nini huzima moto ghafla chumbani?

Hujambo shangazi? Kuna jambo ambalo limenitatiza kwa muda na nimeamua kukuuliza ili nipate kulielewa. Je, ni kitu gani kinachomfanya mwanamume apoteze hisia ghafla wakati wa shughuli za chumbani hata ashindwe kabisa kuzitekeleza?

Kupitia SMS

Kuna sababu tofauti zinazoweza kusababisha hali hiyo. Mojawapo ni iwapo mwanamume huyo ana mpenzi wa pembeni kisha aanze kumfikiria wakati wa shughuli hiyo. Pili, hali hiyo inaweza kutokea kama mapenzi yake kwa mwenzake si ya dhati. Hali hiyo pia inaweza kumpata mtu kutokana na matatizo ya kiafya.

 

Moyo haujamkubali kabisa, shida nini?

Kwako shangazi. Nilikuwa na mpenzi na tukaachana nikiwa na mtoto wake. Baadaye nilipata mwingine ambaye nilikuwa na matumaini kwake kwamba atanioa ili mtoto wangu apate mtu wa kumuita baba. Miaka mitatu baadaye nilimuacha nilipogundua kuwa ana familia na hakuwa ameniambia. Sasa nimepata mwingine mahali ninakofanya kazi na anataka kunioa. Shida ni kuwa tunapokuwa pamoja fikira zangu huwa haziko kwake. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ninaona kwamba unapenda sana maisha ya ndoa na ndiyo maana hujakata tamaa na bila shaka hatimaye utaolewa uweze kutulia na kuridhisha moyo wako. Ninavyokuelewa ni kwamba unampenda uliye naye lakini unakawia kumfungulia moyo wako. Ninaamini hali hiyo inatokana na hofu kwamba anaweza kukutendea ulivyotendewa na wengine. Ushauri wangu ni kuwa uende taratibu usije ukajipata tena katika hali hiyo. Jipe muda umchunguze kwanza hadi utakapotosheka kwamba anakupenda na ana nia nzuri kwako ndipo umruhusu kuingia katika maisha yako.