Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Amezidi kwa ngoma hata nikiugua hanipi nafasi!

February 18th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI natumai wewe ni mzima. Mimi pia ni mzima, nashukuru. Nina mpenzi tunayependana sana lakini ana tatizo moja tu. Anapenda sana shughuli za chumbani kiasi kwamba hunilazimisha hata nikiwa mgonjwa. Tumegombana mara nyingi kuhusu tabia yake hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Maelewano na hali ya mtu kumjali mwenzake ni miongoni mwa nguzo kuu za uhusiano wa dhati. Ikifikia hali ya mtu kudai huduma kwa lazima hata mwenzake akiwa mgonjwa, hayo si mapenzi bali ni tamaa na ubinfasi. Bila shaka hayo ndiyo maumbile yake na sidhani atabadilika. Hiyo ina maana kuwa ukimuoa mtaendelea kugombana tu. Kama unahisi huwezi kuvumilia hali hiyo, ni heri umwambie ili muachane.

 

Mpenzi alihamia kazi mjini sasa nahisi ameoa ila anadai bado ni mie tu

Shikamoo shangazi! Mpenzi wangu alipata kazi mjini miezi miwili iliyopita. Amekuwa akinipigia simu kunihakikishia kuwa bado ananipenda. Lakini nimepata habari kutoka kwa rafiki yake wa karibu kwamba amemuona mara kadhaa na mwanamke mwingine. Juzi nilimpigia simu ikapokewa na mwanamke aliyedai kuwa mke wake. Nilipomuuliza mpenzi wangu alidei eti wao ni marafiki tu hajamuoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Huhitaji maelezo zaidi kujua kwamba mpenzi wako amepata mwingine. Rafiki yako alikwambia kuwa amekuwa akimuona na mwanamke mwingine na wewe mwenyewe ukathibitisha ulipopiga simu ikapokewa na mwanamke. Isitoshe, mpenzi wako pia amethibitisha ingawa anadai eti huyo ni rafiki tu. Uongo mtupu! Kama bado unafikiria una mpenzi unajidanganya.

 

Sina mpenzi lakini hupandwa na hamu je, naweza kuathirika kwa kutohudumiwa?

Vipi shangazi? Tafadhali nimekuja kwako kwa ushauri kuhusu jambo linalonitatiza moyoni. Nina umri wa miaka 22 na sijawahi kuwa na uhusiano na mwanamume yeyote. Nimekuwa nikipandwa sana na hisia za kushiriki mahaba lakini ninavumulia tu. Je, ninaweza kuwa na tatizo lolote nikikosa huduma hiyo?

Kupitia SMS

Sijawahi kusikia kuhusu matatizo yoyote yanayoweza kumpata mtu kwa kutoshiriki mahaba. Wewe sasa ni mtu mzima na ni jambo la kawaida kuwa na hisia hizo mara kwa mara kwa sababu mwili unahitaji. Lakini kama hujapata wa kukuhudumia, endelea kuvumilia tu hadi utakapompata.

 

Wanaume wawili wametangaza penzi lao kwangu sijui nikubali yupi kati yao

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 29 na sina mpenzi. Kuna wanaume wawili ambao wananipenda sana na nimeshindwa nitachagua nani kati yao. Naomba ushauri.

Kupitia SMS

Mpenzi au mume ni chaguo na moyo wa mtu binfasi. Ninaamini unawajua vizuri wawili hao na pia unajua moyoni mwako aina ya mpenzi na mume unayetaka kuwa naye maishani. Tumia kipimo hicho cha moyo wako kuchagua mmoja.

 

Nimpendae anadai mie ni kinyangarika nimejaa wanaume na hilo limeniuma sana

Shikamoo shangazi! Mwanamume mpenzi wangu aliniacha kwa kushuku kuwa sikuwa mwaminifu kwake. Alidai eti nimekuwa na msururu wa wanaume katika mtaa ninamoishi. Ukweli ni kuwa alikuwa mpenzi wangu wa kwanza na nilimpenda kwa dhati. Madai yake hayo yameathiri vibaya hisia zangu hata sijui kama nitawahi kumpenda mwanamume mwingine. Nahitaji ushauri wako tafadhali.

Kupitia SMS

Inashangaza kwamba mpenzi wako huyo alikulaumu na kukuacha kwa madai ambayo hayakuwa na msingi. Hatua kama hiyo inaweza tu kutekelezwa na mtu ambaye, kwa sababu zake mwenyewe, ameamua kujiondoa katika uhusiano kwa vyovyote vile. Kwa sababu hiyo, atakusingizia mambo mabaya zaidi ambayo hayana msamaha bali dawa yake pekee ni kuachana. Bila shaka ametimiza nia yake. Ushauri wangu ni kuwa ujipe moyo kwani huo si mwisho wa maisha. Hatimaye majeraha aliyokusababishia yatapona na umpate mwingine anayestahili penzi lako.