Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ananipenda lakini ni mume wa mwenyewe, itakuwaje?

November 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shagazi? Nina umri wa miaka 22. Kuna mwanamume fulani ambaye ananipenda sana na mimi pia nampenda. Ananisaidia kwa mambo mengi lakini naogopa kwa sababu ni mume wa wenyewe. Isitoshe, anataka tushiriki mahaba ilhali mimi bado ni mdogo na sijui mambo hayo. Nishauri.

Kupitia SMS

Wewe ni msichana mdogo sana kiumri na utajiharibia maisha ukiingia kwenye mtego wa mwanamume huyo. Labda anakushawishi kwa pesa lakini nakuonya kuwa huo ni uhusiano hatari. Kama unahitaji mpenzi, tafuta mwanaume wa rika yako ambaye anaweza kukuoa.

 

Nilimuacha sasa namtamani sana ila naogopa kumuelezea

Hujambo shangazi? Nilikuwa na mwanamume mpenzi wangu tuliyependana sana lakini nikaamua kumuacha bila sababu. Sasa nimeingiwa na upweke na natamani sana turudiane kwa sababu alinipenda kwa moyo wake wote lakini naogopa kumwambia. Nishauri.

Kupitia SMS

Unafaa kujilaumu mwenyewe kwa kumuacha mpenzi wako bila sababu. Hata ukipata ujasiri wa kumwelezea unavyohisi, huenda nia yako ikatibuka kwani huenda ameshapata mwingine. Lakini usife moyo, huenda bado hajapata na bado anakupenda. Mtafute umwambie ndipo ujue msimamo wake.

 

Nataka kuoa lakini wote ninaochumbia hawataki kuishi mashambani

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 27 na nimekuwa nikitafuta mke kwa muda sasa lakini bado sijapata. Wanawake ambao nimekutana nao nikitaka kuwaoa hawataki kuishi mashambani wanataka tuishi mjini. Mapato yangu ni madogo na siwezi kugharamia maisha ya familia mjini. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama unatafuta mke mjini na unataka aishi mashambani, basi utaambulia patupu. Mwanamke ambaye amezoea maisha ya mjini hawezi kuishi mashambani. Kama unataka mke wa kuishi mashambani, itabidi umtafute huko huko mashambani ambako amezoea kuishi.

 

Wakwe hawanitaki kwa kuwa natoka familia maskini

Shangazi nahitaji ushauri wako. Nimekuwa na mchumba kwa miaka miwili na wazazi wangu wamekubali anioe. Tulifunga ndoa majuzi tu lakini wazazi wake wamepinga ndoa yetu kwa sababu ninatoka familia maskini. Licha ya hayo mume wangu ananipenda. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba mume wako ni mtu mzima kwa hivyo ana haki ya kufanya maamuzi kuhusu maisha yake. Wazazi wake wanakosea kwa kupinga ndoa yenu kwa sababu hawana haki ya kufanya hivyo. Ushauri wangu ni kuwa msiwape nafasi hiyo. Isitoshe, unasema mume wako anakupenda kwa hivyo huna sababu ya kuwa na wasiwasi.

 

Nina mpenzi ambaye yuko kazini na mimi mwanafunzi wa upili

Vipi shangazi? Ninasoma shule ya upili na nimekuwa na uhusiano na mwanamke anayefanya kazi kwa miezi kadhaa sasa. Wazazi wangu wamegundua na wanapinga vikali uhusiano huo. Nampenda sana mwanamke huyo, sijui nitafanya nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa wazazi wako wanapinga uhusiano huo kwa sababu wanahofia utaathiri vibaya masomo yako. Huwezi kamwe kuchanganya masomo na mapenzi kwa hivyo nakushauri ukubali na kutii msimamo wa wazazi wako iwapo unajali maisha yako ya baadaye.

 

Mume yuko katika uhusiano na mke wa mtu

Shikamoo shangazi! Nimegundua kuwa mwanamume mpenzi wangu ana uhusiano na mwanamke mwingine tena mke wa mtu. Nilipashwa habari hizo na rafiki yangu na nilipokagua simu yake nikapata SMS za kimapenzi kutoka kwa mwanamke huyo. Alishtuka sana nilipomuuliza juzi na akaondoka tu bila kusema chochote. Nampenda sana, sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Umejua kwa hakika kuwa mwanamume huyo si mwaminifu kwako kwa hivyo hakuna haja ya kuendelea kupoteza wakati wako ukimfikiria. Ni bahati kwamba umejua mapema kabla hujakuoa kwani ingekuwa balaa ukijua tabia yake hiyo akiwa mume wako.