Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Anataka kunioa ila SMS za wapenzi wake zanitia hofu

September 28th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 26. Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani kwa mwaka mmoja sasa na ameahidi kunioa. Tulipokutana aliniambia alikuwa na wapenzi kadhaa hapo awali na wakaachana. Lakini nimechunguza nikagundua kuwa bado huwa anawasiliana nao kwa simu. Mara nyingi wanamtumia SMS na nikimuuliza anasisitiza kuwa waliachana. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hizo ni dalili kwamba mwanamume huyo bado hajakata kauli kuhusu uhusiano wenu ingawa unasema ameahidi kukuoa. Ushauri wangu ni kwamba umwelezee wazi kuwa hutaweza kumvumilia akiendelea kuwasiliana na wapenzi wake wa awali. Asipojirekebisha, itabidi uachane naye kama hutaki kuvunjika moyo mara kwa mara kutokana na tabia yake hiyo.

 

Anashikilia mimba ni yangu ila ninaamini si yangu hata kidogo

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 23 na nimekuwa na mpenzi kwa miezi kadhaa. Tunafanya kazi katika miji tofauti lakini nimekuwa nikimtembelea mara kwa mara. Nimeshangaa baada ya mpenzi wangu kuniambia kuwa ana mimba. Ninaamini kuwa mimba hiyo si yangu kwa sababu tumekuwa tukitumia kinga na nimemwambia tuachane. Lakini amekataa akisisitiza kuwa ni yangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Jinsi pekee ya kujua ukweli wa jambo hilo ni kusubiri hadi mtoto atakapozaliwa kisha mfanyiwe ukaguzi wa kitaalamu kuthibitisha iwapo ni wako au la. Badala ya kumpuuzilia mbali mpenzi wako ukimwambia muachane, shauriana naye mkubaliane kuwa mtoto akizaliwa mtapimwa na ikithibitishwa si wako basi muachane.

 

Mume wangu haachi kuwavizia wajakazi

Shikamoo shangazi! Nimeolewa lakini nina shida katika ndoa yangu. Mume wangu ana tabia ya kutongoza wafanyakazi wa nyumbani kwetu. Nimemfumania mara kadhaa na kumsamehe lakini sasa ninahisi siwezi kuvumilia tena tabia yake hiyo. Nimejitahidi sana kumuonyesha mapenzi ya kutosha lakini hataki kujirekebisha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ndoa ni uhusiano unaotokana na mapenzi na maelewano kati ya mume na mke. Kuna mambo na hali nyingi zinazoweza kuvumiliwa ili kudumisha ndoa isipokuwa tu ukosefu wa uaminifu. Ni aibu kubwa na kukukosea heshima kwa mume wako kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wasichana wa kazi. Utaitesa nafsi yako kwa kuendelea kuvumilia mambo kama hayo na ushauri wangu ni kwamba ujiondoe katika ndoa hiyo ujitafutie maisha mengine.

 

Kumbe ana mtoto na hajawahi kuniambia!

Habari za kwako shangazi? Nimegundua kuwa mwanamke mpenzi wangu wa miaka mitatu ana mtoto na hajawahi kuniambia. Jambo hilo limeniudhi sana na sijui nitafanya nini kwa sababu ninampenda sana na hata nimemtambulisha kwa wazazi na jamaa zangu wengine kuwa ndiye ninayepanga kuoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Baadhi ya wanawake waliopata watoto kabla ya kuolewa huweka jambo hilo kuwa siri kwa kuhofia kukosa wachumba. Huenda hiyo ndiyo sababu mpenzi wako hakukwambia kuwa ana mtoto. Kama unahisi yeye ndiye chaguo lako maishani, mkubali pamoja na mtoto wake.

 

Japo nilimwacha kwa sababu ya ukware wake, bado nampenda

Shikamoo shangazi! Tafadhali naomba ushauri wako. Nilikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani lakini nikamuacha alipoanza kunionyesha dharau kwa kutongoza wanawake wengine mbele yangu. Ni miaka miwili sasa tangu nimuache na nimeshindwa kabisa kumsahau kwa sababu ninampenda kwa dhati. Je, nimtafute turudiane?

Kupitia SMS

Ninahisi kuwa mwanamume huyo alitosheka na penzi lako na kwamba hatua yake ya kuwatongoza wanawake wengine ukiwepo ilinuiwa kukuchukiza ili umuache na hatimaye uliingia katika mtego wake. Sielewi ni kwa nini unataka kujilazimisha kwake licha ya kukutendea hayo. Huenda hata akakutendea mabaya zaidi. Hata kama unampenda, itabidi ukubali kwamba huna nafasi katika moyo wake na utafute mapenzi kwingine.